Meneja wa Fedha na Utawala BOT Mkoa wa Mtwara Bw.David Mponeja akifungua semina ya waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha katika tawi la Benki Kuu Mtwara kwa niaba ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw.Julian Banza leo Mkoani humo. Waandishi wa habari wakifuatilia semina inayohusu waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha uliofanyika leo katika ukumbi wa mkutano katika tawi la Benki Kuu Mtwara.
Mkuu wa Maendeleo ya Uchumi BOT Bw.Mussa Mziya akiwasilisha Mada katika Semina ya waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha uliofanyika leo katika tawi la Benki Kuu Mtwara.
*********************************
NA EMMANUEL MBATILO, MTWARA
Wanahabari wametakiwa kutumia kalamu na vyombo vyao kuelezea mipango ya kuelekea uchumi wa viwanda, changamoto na namna ya kuzitatua ili kuwezesha wananchi kupata taarifa sahihi.
Ameyasema hayo leo Meneja wa Fedha na Utawala BOT Mkoa wa Mtwara Bw.David Mponeja akifungua semina ya waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha katika tawi la Benki Kuu Mtwara kwa niaba ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw.Julian Banza leo Mkoani humo.
Akizungumza wakati akifungua semina hiyo Bw.Mponeja amesema kuwa wananchi wanataka kujua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi ambayo ikikamilika itachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa letu na jinsi kila mmoja wetu anavyoweza kuchangia kuhakikisha Tanzania siyo tu inaendelea kuwa katika nchi za uchumi wa kati, bali inazidi kusonga mbele kimaendeleo.
“Tumieni weledi wenu kuwafahamisha wananchi hatua mbalimbali ambazo awamu ya pili ya Serikali ya Awamu ya Tano inazichukua katika kuwatumikia. Msiache kuwaelezea wananchi hatua ambazo miradi ya kimkakati kama reli ya kisasa (Standard Gauge Railway), mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga na mradi wa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme katika katika Mto Rufiji imefikia na faida ambazo taifa litapata ikishakamilika”. Amesema Bw.Mponeja kwa niaba ya Naibu Gavana Bw.Banza.
Aidha pamoja na hayo amewahimiza wananchi mmoja mmoja na vikundi vinavyotoa au vinavyotaka kutoa huduma ndogo za fedha kujisali na kujiandikisha kwa mamlaka mbalimbali kwa mujibu ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.
Pamoja na hayo amesema Benki Kuu itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha taarifa muhimu zinazotakiwa ziwafikie wananchi kutoka katika vyombo vya habari zinawafikia.