Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw. Richard A. Kasesela akizungumza na Mkurugenzi wa udhibiti ubora TBS Bw. Lazaro Msasalaga (wa pili kushoto), Kaimu Mkuu wa kanda ya nyanda za juu kusini TBS Bw. Abel Mwakasonda pamona na Mchumi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bi. Chresencia Mwimbwa walipoenda kumtembea ofisini kwake kabla ya kuanza kwa mafunzo kwa wadau wa mafuta ya kula Iringa. Maafisa wa TBS wakitoa elimu juu ya uhifadhi na ufungashaji bora wa mafuta ya kula kwa muuzaji katika soko mkoani Iringa.
**************************************
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard A. Kasesela, ameagiza viongozi wa Halmashauri za wilaya kuanzisha maeneo maalum ya kusindikia bidhaa ili kuwezesha wajasiriamali wadogo kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi matakwa ya viwango.
Mhe. Kasesela aliyasema hayo wakati wa akifungua rasmi mafunzo kwa wadau wa mafuta ya kula mkoani Iringa ambapo yanategemea pia kuhusisha mikoa ya Njombe na Mbeya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa TBS Bw. Lazaro Msasalaga, alisema kuwa ili mafuta yakidhi viwango ni lazima kufuata kanuni bora za kilimo ikiwemo kutumia mbegu bora na kuvuna kwa wakati, kanuni bora za usindikaji na kanuni bora za afya ikiwemo uhifadhi wa mafuta ya kula katika eneo ambalo halipigwi na jua kwani kwa kufanya kinyume na hivyo itasababisha kuzalishwa kwa kemikali zisizofaaa kwa binadamu katika mafuta hayo na kusababisha madhara makubwa ikiwemo magonjwa.
Bw. Msasalaga alisisitiza zaidi ni lazima kufuata kanuni hizo kwa pamoja na siyo kutegemea kanuni ya eneo moja tu kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha bidhaaa kutokidhi matakwa ya viwango.
Naye Kaimu Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa TBS Bw. Abel Mwakasonda, alitoa elimu kuhusu taratibu za uthibitishaji wa bidhaa na usajili wa bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi ambapo aliwaasa wenye majengo na bidhaa zote zinazotakiwa kusajiliwa wafanye hivyo haraka kabla hatua kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Mafunzo haya yamehusisha pia Taasisi mbalimbali ikiwemo SIDO, Wakala wa Vipimo, BRELA pamoja na Maafisa Biashara, Afya na Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri husika.
TBS tayari imekwishatoa elimu ya aina hii awamu ya kwanza katika kanda ya kati ambayo ilihusisha wilaya zilizopo mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora ambapo wadau zaidi ya 1700 walifikiwa na awamu ya pili ilihusisha mkoa wa Kigoma ambapo wakulima, wasindikaji na wauzaji zaidi ya 2000 walifikiwa.