Mratibu wa TAMWA ZNZ ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa akifungua kikao cha mtandao wa kupinga udhalilishaji wilaya ya Mkoani
Wajumbe wa mtandao wakiendelea na kikao
Haji Shoka, mjumbe wa mtandao huo akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya mtandao huo.
************************************
WAJUMBE wa mtandao wa kupinga udhalilishaji wa kijinsia Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba wamesema kuwepo kwa baadhi ya wazazi kuendekeza tamaa ya pesa kwenye kesi za udhalilishaji ni tatizo linalopelekea wadhalilishaji kuendelea kutekeleza matukio hayo katika jamii.
Wameyabainisha hayo wakati wa kikao cha kujadili ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo kwa kipindi cha kuanzia mwezi wa January hadi February kilichofanyika katika ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) Pemba.
Wamesema watekelezaji wa vitendo hivyo wengi wao wanaendelea kutekeleza matukio hayo kwa kutumia uwezo wao kifedha kuwalaghai wazazi wa waathirika kwa kutaka kuwalipa fidia ili kufanya suluhu jambo ambalo linahatarisha zaidi usalama wa waathirika wenyewe na jamii kwa ujumla.
Mjumbe wa mtandao huo, Haji Shoka alisema kutokana na familia nyingi zinazokumbwa na kadhia hiyo kuwa katika hali duni ya maisha jambo hilo limepelekea watekelezaji wa vitendo hivyo kuichukulia kama fursa ya kuendelea kuwadhalilisha bila kujali athari wanazokabiliana nazo waathirika.
“Tamaa ya pesa kwa baadhi ya wazazi kutokana na hali zao za maisha ni tatizo kubwa linalopelekea wadhalilishaji kuendelea kutekeleza matukio haya. Kuna kesi moja tuliifuatilia ya mtoto wa darasa la sita lakini baba mtoto alitaka mtuhumiwa alipe faini ya shilingi milioni mbili ili wayamalize kifamilia. Hadi sasa kwa taarifa zilizopo kashachukua milioni moja na laki nane. Kwahiyo hili ni tatizo kubwa sana”- Haji Shoka, Mwanamtandao wa kupinga udhalilishaji.
Kwa upande wake Salma Majid mmoja wa wajumbe hao amesema licha ya juhudi zinazochukuliwa na mtandao huo lakini bado ucheleweshaji wa kesi za udhalilishaji unapelekea jamii kukosa Imani na wadau wa kupambana na vitendo hivyo kwa kuamini kuwa wanapotezewa muda.
“Ucheleweshaji wa kesi mahakamani huleta tabu kwa jamii na kuona kwamba sisi wadau wa kupambana na udhalilishaji tunapokwenda kufuatilia matukio katika jamii ni kama tunawapotezea muda kwani hawaoni kesi hizo zikipatiwa huku kwa haraka,” amesema.
Aidha aliongeza kuwa kumekuwa na changamoto ya baadi ya wazazi kutokuamini taarifa kuhusu watoto wao pale inapotokezea kafanyiwa vitendo vya udhalilishaji jambo ambalo hupelekea kuchelewa kuchukua hatua kwa wakati.
Alisema, “baadhi ya wazazi ni wagumu na hawaamini wanapopewa taarifa za watoto wao kuhusu tukio la udhalilishaji na hii inapelekea madhara zaidi kwa waathirika na wakati mwingine kutokana na ucheleweshaji wa kuchukua hatua inasababisha hadi mtuhumiwa kupata mwanya wa kukimbia.”
Aliongeza “endapo wazazi watakuwa tayari kutoa mashirikiano kwa wadau na vyombo husika kuchukua hatua mara moja pale linapotokezea tukio ni wazi kwamba itasaidia kupunguza athri kwa mwathirika pamoja na kufanikisha mtuhumiwa kukamawa kabla hajatoroka.”
Nae mratibu wa TAMWA ZNZ ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa alisema ni wakati kwa mtandao kujipanga kwa binu mpya za kukabiliana na wimbi la watuhumiwa kutoroka ikiwa ni pamoja na kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuripoti kwa wakati ili hatua zichukuliwe mapema.
“Tujipange upya kukabiliana na wimbi hili kwani tunafahamu kwamba kesi nyingi za udhalilishaji zinashindwa kupatiwa hukumu kutokana na watuhumiwa wengi kukimbia, na chanzo kikubwa cha watuhumiwa hawa kukimbia ni kutokana na kuchelewa kuchukuliwa hatua pale tu tatizo linapotokea,” alisema.
Aliongeza kuwa, “Pamoja na kwenda kwa jamii zaidi, tuwaelimishe sana kwamba wasiende kuzipeleka kesi za udhalilishaji kwa masheha kusuluhisha na badala yake waziripoti kwenye vyombo huzika ikiwemo kwa maafisa dawati ili hatua ziweze kuchukuliwa na watuhumiwa wahukumiwe kwa mujibu wa sheria.”
Kikao hicho ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa kupambana na udhalilishaji Zanzibar unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kupitia fadhili wa ubalozi wa Finiland.