****************************************
18 Februari 2021, Dar Es Salaam: Kampuni ya simu za mkononi inayoongoza nchini nchini, Vodacom Tanzania PLC leo imetangaza gawio la jumla ya shilingi bilioni 4.1 kwa wateja wa M-Pesa ambao wametumia huduma hiyo kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba mwaka jana.Hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.37 ukilinganisha na gawio lililopita.
Akiongea juu ya gawio hili, Mkurugenzi wa M-Pesa Epimack Mbeteni alisema kuwa faida hii iliyoanza kulipwa tangu tarehe 15 Februari, inalipwa kwa wateja, mawakala na washirika wa biashara wa M-Pesa ambao wametumia huduma ya M-Pesa kwa kipindi tajwa.
“Kutokana na utaratibu na kanuni za Benki Kuu ya Tanzania, faida inayopatikana kutokana na uwekaji wa fedha huwa inarejeshwa kwa mteja aliyetumia huduma hizo. Leo tuna furaha kuutangazia umma kwamba tutagawa shilingi Bilioni 4.1 kwa wateja wetu zaidi ya milioni 11 kote nchini. Huduma yetu ya M-Pesa kupitia simu za mkononi inaendelea kuongeza thamani kubwa ya fedha kwa Watanzania. Tumeona ukuaji mkubwa kwenye matumizi ya M-Pesa na ongezeko la Wateja, mawakala, wafanyabiashara na taasisi zinazofanya biashara hadi kufikia mzunguko wa zaidi ya Shilingi bilioni 100 kila siku,’ alisema Mbeteni.
Hadi sasa kampuni hiyo imelipa jumla ya shilingi 147.6 bilioni ikiwa ni faida iliyolipwa tangu Julai 2015 wakati Benki Kuu ya Tanzania ilipopitisha kanuni hiyo.
Faida kwa kila mteja inahesabiwa kulingana na kanuni za Benki Kuu ya Tanzania na itategemea, pamoja na mambo mengine, kiwango cha matumizi ambayo wateja wa M-Pesa wamefanya kwa kipindi hicho.
“Tunawalipa wateja wetu wa M-Pesa kupitia akaunti zao. Wateja wanaweza kutuma neno AMOUNT/KIASI kwenda 15300 kwa ujumbe mfupi ili kujua ni kiasi gani cha faida watakachopokea. Baada ya kupokea kiasi kilichotolewa, wateja wa M-Pesa wanaweza kutumia faida hiyo kununua muda wa maongezi au manunuzi ya vifurushi au hata kulipia bili au kununua bidhaa,” aliongeza Mbeteni.
Huduma ya Vodacom M-Pesa ni ya ubora wa juu zaidi nchini, ikiwa ni bidhaa iliyotengenezwa ili kuongeza ujumuishwaji wa kifedha nchini, huku ikichochea shughuli za kiuchumi nchini kote. Bidhaa zingine ni pamoja na; Songesha ambayo ni huduma ya mkopo ya muda mfupi, M-Koba ambayo ni akaunti ya akiba ya kikundi, Lipa Kwa Simu ikiruhusu miamala ya mteja kulipia bidhaa, M-Pawa ambayo ni jukwaa la akiba na mikopo na mengineyo zaidi.
“Tutaendelea kuongoza katika ubunifu ili kuleta Watanzania wengi katika uchumi jumuishi wa kidijitali, kuongeza idadi ya wateja wanaotumia huduma ya M-Pesa kupitia simu za mkononi na kupanua huduma zetu za biashara, tukizingatia ushirikiano wa kimkakati na kudumisha aina anuwai za huduma ambazo zitaturahisishia malipo kuwa ya haraka, rahisi na salama kwa Wafanyabiashara na watu binafsi,” alihitimisha Mbeteni.
Kuhusu Vodacom M-Pesa Tanzania
Vodacom M-Pesa ni huduma ya kifedha kwa njia ya simu inayoongoza nchini iliyoanzishwa na Vodacom Tanzania PLC mwaka 2008. Kwa sasa ni moja ya huduma chache duniani zilizopewa tuzo ya ubora ya GSMA na ina wateja zaidi ya milioni 11. Kwa kiasi kikubwa M-Pesa imechangia katika kukua kwa huduma za kifedha na shughuli za uchumi nchini. Wateja wanatuma na kuweka pesa kupitia huduma ya M-Pesa kupitia kwa mawakala zaidi ya 106,000 nchini kote. Mfumo wa M-Pesa unaunganisha mabenki, makampuni na mashirika ya Serikali katika kufanya malipo ya kidigitali.
Kwa sasa, M-Pesa inaendelea kuwa kinara katika soko la huduma za kifedha nchini kupitia huduma zake za kibunifu kama vile Akiba na Mikopo, malipo ya kieletroniki, huduma za vikundi na nyingine nyingi ambazo zinakidhi mahitaji ya watanzania na kuwezesha ufikaji na utumiaji Zaidi wa huduma rasmi za kifedha.