Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) akitoa shukrani zake kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli mara baada
ya kukabidhiwa hati ya eneo lake.
Na John Mapepele, Manyoni
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi ametekeleza agizo ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilomtaka
kushirikiana na Viongozi wa Wilaya ya Manyoni kumrejeshea umiliki wa eneo lililokuwa mali ya Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) ambaye
lilichukuliwa na Afisa Ardhi aitwaye Leonard Msafiri na kisha kupangishwa kwa Kampuni mmoja ya simu za mikono ambayo imeweka mnara wa mawasiliano lirejeshwe mara
moja kwa mama huyo ambaye ndiye
ataingia mkataba wa upangaji na Kampuni hiyo.
Akikabidhi hati ya umiliki wa
ardhi wa miaka 66 wa eneo hilo la Majengo Kiwanja Na 13 hivi karibuni Mkuu wa
Mkoa wa Singida Mhe, Dkt. Rehema Nchimbi
amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Mhe, Dkt. John Pombe
Magufuli ina dhamira ya dhati ya kuwasaidia wananchi wanyonge ili wapate
haki zao na kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo ili kuchangia katika
uchumi wa kati na hatimaye uchumi wa juu wa Taifa letu.
Amesema Mkoa umejipanga kimkakati kuhakikisha kuwa migogoro yote ya
ardhi inakwisha mara moja kwenye Mkoa wa
Singida na kuagiza Wakuu wote wa Wilaya na Wataalam wa ardhi kuanzia sasa kutatua migogoro ya ardhi katika
maeneo husika badala ya kufanya mashauri ya migogoro ya ardhi maofisini.
“Kuanzia leo sitaki kuona shauri na migogoro ya ardhi ikitatuliwa maofisini, naagiza wakuu wote wa Wilaya
katika Mkoa wangu na wataalam kwenda
moja kwa moja kutatua migogoro ya ardhi ya wananchi katika maeneo ya migogoro, hatua kali
zitachukuliwa kwa wote ambao hawatatekeleza
agizo hilo” alisisitiza Mhe. Nchimbi
Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya
Manyoni amesema ni lazima iishe mara moja kwa
kuwa Manyoni ya sasa ni Sebule ya
Makao Makuu ya nchi-Dodoma na kwamba watu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania
wanakuja Manyoni kwa kuwa kuna maeneo mazuri yenye fursa za uwekezaji hususan
kwenye viwanda, biashara na kilimo cha zao la Korosho ambapo kwa sasa
Wilaya hii inaongoza siyo tu Tanzania bali katika Bara la Afrika kwenye kilimo hicho ambapo
kumekuwa na shamba la pamoja la Kilimo cha Korosho (Block Farming)lenye takribani ekari 25000.
“Haiwezekani Manyoni hii ambayo ni lango la makao makuu ya nchi ikaendelea kuwa na migogoro ya
ardhi ambapo sasa ardhi yake imebeba
uwekezaji mkubwa katika nchi yetu” aliongeza Mhe. Mkuu wa Mkoa
Akipokea hati yake ya umiliki wa
eneo hilo, Bibi Elizabeth Msalali
alimshukuru Rais Magufuli kwa kusaidia kupatikana kwa kiwanja chake
ambapo amesema Magufuli ameonyesha kuwa
ni Rais anayewapigania watu masikini na
wanyonge kama yeye hivyo anamwombea kwa Mungu azidi kumbariki katika utumishi
na maisha yake kwa ujumla.
Aidha Mtoto wa pekee wa Bi Elizabeth ambaye ndiye aliyemwomba Mhe. Rais
Magufuli kuingilia kati suala hili Bwana, Adamu Kazimoto alimshukuru na
kumpongeza Mkuu wa Mkoa, Dkt. Rehema Nchimbi kwa kuharakisha kukamilisha
mchakato wa kupata hati ya
umiliki wa kiwanja hicho kwa mama yake
ambapo amesema mchakato huo umechukua
muda mfupi sana.
“Naomba niwe mkweli kama tungekuwa na fedha ya kulipia hiki kiwanja
nadhani ingechukua siku
moja au mbili tu baada ya agizo la Mhe.Rais maana Kamishina Msaidizi wa
Mkoa wa Singida Dada Shamimu Hoza alikamilisha
utengenezaji wa hati hiyo mara moja baada ya tamko hilo la Mhe.Magufuli jambo ambalo limetupa
faraja kubwa kwani sasa mama yangu amepata
haki yake” ameongeza Adamu
Akifafanua Adamu amesema suala hili
alianza kufuatilia zaidi ya miaka
tisa iliyopita, na anamshukuru Rais Magufuli kwa kutoa suluhisho la kudumu ambapo pia
ameongeza kwamba mgogoro huo umeifanya familia ya Mzee Kazimoto kuwa kitu
kimmoja licha sintofahamu ambazo zilikuwepo hapo awali kwa sababu ya tamaa ya
pesa kwa wanafamilia.
Mhe. Rais John Pombe Magufuli
alilitoa agizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kushughulikia mgogoro huo tarehe 31Januari 2021 aliposimama
kuwasalimu wananchi wa Manyoni wakati akiwa safarini akitokea Tabora kwenda
Dodoma.
Rais Magufuli alisikiliza kero inayowakabili wananchi hao ambao
walilalamikia kitendo cha Idara ya Ardhi
kuchukua maeneo yao bila kuwalipa fidia na wengine kuamriwa kuondoka katika eneo hilo baada ya kupewa nyaraka za kupatiwa
radhi(offer) hali iliyozua mgogoro kati ya wamiliki wa asili wa eneo
hilo na Idara ya Ardhi.
Rais ameagiza wananchi wenye offer
waruhusiwe kuendeleza maeneo waliyopatiwa na wamiliki wa asili wa eneo
hilo kulipwa fidia kwa mujibu wa Sheria.
Awali, kufuatia agizo la
Mheshimiwa Rais, Timu Maalum ya wataalam kutoka Mkoani na Wilaya ya Manyoni
iliyoongozwa na Kamishina Msaidizi wa Mkoa wa Singida Shamimu Hoza Shaban
ilikutana familia nzima ya mmiliki wa
asili wa eneo hilo marehemu Salum
Kazimoto aliyefariki mwaka 1973
ambayo ilikuwa inavutana
kuhusu umiliki wa eneo hilo ambapo
baada ya majadiliano ilikubaliana
kwa kauli mmoja kwamba mmliki halali wa
eneo hilo ni Bibi Elizabeth Msalali.
Kutokana na Wilaya ya Manyoni kuonekana kuwa na migogoro
ya ardhi kadhaa ya ardhi kwa muda mrefu sasa, mkakati maalum wa kusikiliza kero
hizo umeandaliwa ambapo timu ya wataalam
na viongozi wa Halmashauri hiyo unazungukia katika maeneo husika ili
kuhakikisha migogoro yote inaisha kama
ilivyoamriwa.