Home Mchanganyiko MAMLAKA YA HALI YA HEWA TMA YATANGAZA UTABIRI WA MVUA ZA MASIKA...

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TMA YATANGAZA UTABIRI WA MVUA ZA MASIKA KUANZIA MACHI MPAKA MEI 2021

0

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA na (Kaimu Mkurugenzi Mkuu), Dkt. Hamza Kabelwa akitangaza utabiri wa hali ya hewa kwa kipindi cha mvua sa Masika kinachoanzia Machi mpaka Mei.

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA na (Kaimu Mkurugenzi Mkuu), Dkt. Hamza Kabelwa katikati akizungumza wakati akitangaza utabiri huo kushoto ni Dkt. Kantamla Mafuru Mkuu kitengo cha uchambuzi wa utabiri na kulia ni Samwel Mbuya ,Meneja kituo kikuu cha utabiri.

Joyce Makwata mchambuzi wa hali ya hewa akifafanua jambo wakati mamlaka hiyo ilipotangaza utabiri wa mvua za Masika kuanzia Machi mpaka Mei 2021.

………………………………….

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA na (Kaimu Mkurugenzi Mkuu), Dkt. Hamza Kabelwa  ametangaza taarifa ya  utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa mvua za Masika ambao ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), Pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).

Maeneo mengine ikiwa ni ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. 

Dk Kabelwa amesema kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na inavyotarajiwa katika kipindi chote cha msimu (kama ilivyoelezwa katika kipengele cha III cha taarifa hii), kwa ujumla mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

“Hata hivyo, maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa Ziwa Viktoria yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Aidha, maeneo ya pwani ya kaskazini yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Msimu wa mvua za Masika unatarajiwa kuambatana na vipindi vya mvua kubwa hususan katika kipindi cha mwezi Machi”. Amesema Dk. Kabelwa alipotoa taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema katika ukanda wa Ziwa Viktoria: (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kakonko na Kibondo)):

Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mvua hizi zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2021 na kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Mei, 2021.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba):

 Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini. Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza mapema katika wiki ya nne ya mwezi Februari, 2021 na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya tatu ya mwezi Mei, 2021.imesema taarifa hiyo.

Kwa uuande wa Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro) Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuanza mapema katika wiki ya nne ya mwezi Februari, 2021 na kuisha katika wiki ya tatu ya mwezi Mei, 2021.

Katika kipindi cha Masika (Machi hadi Mei, 2021) hali ya unyevunyevu wa udongo na maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji inatarajiwa. Hata hivyo, hali  hiyo ya unyevunyevu hususan katika maeneo ya ukanda wa ziwa Victoria na nyanda za juu kaskazini mashariki yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, inaweza kuathiri ukuaji wa baadhi ya mazao yasiyohitaji maji mengi, kama vile mahindi, maharagwe na mazao ya mizizi.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa , katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, upungufu wa unyevunyevu kwenye udongo unaweza kujitokeza. Inashauriwa kuimarisha miundombinu ya kilimo ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na vipindi vifupi vya mvua kubwa. Teknolojia ya uvunaji maji ya mvua izingatiwe ili kuhifadhi maji kwa matumizi ya baadae. Wakulima wanahimizwa kutafuta na kutumia ushauri wa wataalam wa kilimo ikiwa ni pamoja na maafisa ugani katika maeneo yao.