…………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amesema Serikali haitapoteza muda na wasanii wanaofanya “kiki” badala ya kutumia muda wao vizuri kutengeneza kazi bora zitakazouzika ndani na nje ya nchi kwa manufaa yao na Taifa.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo Febrari 17, 2021 alipokagua majengo yaliyopo Kivukoni jijini Dar es salaam akiwa ameambatana na Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma na Ujenzi wa Mji wa Serikali, Bw. Meshack Bandawe ili kuweza kuyakabidhi kwa Taasisi zinazosimamia Sekta ya Sanaa za COSOTA, BASATA na Bodi ya Filamu, ikiwa ni juhudi za kuziwezesha Taasisi hizo kufanya kazi ndani ya eneo moja na kurahisisha utoaji huduma.
“Serikali kama alivyoahidi Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ipo kazini kuhakikisha sekta ya Sanaa inakua na kutoa mchango chanya kwa vijana. Hapa leo tunapambana ili taasisi zetu hizi zipate ofisi nzuri na kutoa huduma kutoka sehemu moja baada ya malalamiko ya miaka mingi kuwa ziko mbali, lakini unashangaa baadhi ya wasanii wanaturudisha nyuma kwa kufanya kiki badala ya kazi nzuri” alisema Dkt.Abbasi.
Dkt. Abbasi ameongeza kuwa Serikali haitakuwa upande wa wasanii wanaovunja Sheria za nchi na maadili badala yake itakua bega kwa bega na wale ambao wako tayari kufanya kazi nzuri na kuitangaza nchi vizuri.
“Jana nimeletewa habari nyingi sana wengine wamepelekana polisi, wengine unasikia hivi, hawa wanataka kuturudisha nyuma niwaambie Serikali haiwezi kuwaendekeza hao, Nasisitiza hizi ni zama za kazi sio kiki, waambieni hao vijana anayesikia asikie hii ni sauti na amri kutoka Serikali Kuu” alisisitiza Dkt. Abbasi.
Aidha, Dkt. Abbasi amesema kuwa uamuzi wa taasisi hizo kukaa pamoja umeshapitishwa na kilichobaki ni taasisi hizo kugawiwa na kuhamia eneo hilo huku mipango kama hiyo ikiendelea katika Makao Makuu Jijini Dodoma.