Home Mchanganyiko TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI KUFANYIWA MABORESHO

TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI KUFANYIWA MABORESHO

0
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Mvomero leo alipofanya ziara kukagua skimu za umwagiliaji na Kilimo cha miwa Mtibwa ambapo ameagiza kuhakikisha kinatatua tatizo la bei ya miwa.
Waziri wa Kilimo Prof.Adolf Mkenda ( wa pili kushoto) akiwasili Mtibwa kuzungumza na wakulima wa miwa juu ya changamoto za bei 
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akizungumza na wakulima wa miwa wa Mtibwa leo alipofanya ziara Wilaya ya Mvomero. Kushoto ni Katibu Mkuu Kilimo Bw. Gerald Kusaya na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albinius Mgonya.
( Habari na Picha na Wizara ya Kilimo)
……………………………………………………………………………………..
Waziri Kilimo Prof Adolf Mkenda leo ameanza ziara ya kikazi wilayani Mvomero kwa lengo la kukagua  miradi ya umwagiliaji na hali ya uzalishaji sukari kwenye kiwanda  cha Mtibwa pamoja na kuongea na wakulima.
Awali akongea na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero Prof.Mkenda amewataka waendelee kusimamia kazi za kilimo ikiwemo miradi  ya umwagiliaji ili wakulima waongeze  tija na kuweza kulima zaidi ya mara moja kutokana na wilaya hiyo kuwa na maeneo mazuri  kwa umwagiliaji.
Prof. Mkenda alisema wizara yake inapitia upya  utendaji kazi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ikiwemo kutafuta watumishi wenye  weledi wa kubuni  na kusimamia miradi yenye kutoa tija kwa wakulima.
” Suala la umwagiliaji bado lina shida,tunahitaji kulipatia suluhu ya mapema  kwani haiwezekani serikali ijenge miundombinu halafu uzalishaji uwe na tija ndogo na wakati mwingine  wakulima washindwe kutunza miundombinu kama kulipia umeme” alisema Prof. Mkenda
Akizungumza kuhusu sekta ya sukari Waziri Mkenda alisema tayari mkakati wa kuona uzalishaji sukari unaongezeka umeanza kwa kuwataka wawekezaji kutumia fursa ya kilimo cha umwagiliaji kukuza tija na kutumia mbegu bora za miwa.
Aliongeza kusema serikali itaendelea kuweka mazingira sawa ili kuwe na ushindani sawa kwa wawekezaji na nchi izalishe sukari nyingi.
“Nahimiza uwekezaji katika sekta ya sukari na kuwa serikali itasimamia ushindani ili nchi iwe na uhakika wa uzalishaji na hivyo wawekezaji zaidi wanakaribishwa nchini” alisisitiza Mkenda.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albinus Mgonya alisema wilaya  ina eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hekta 77,005 kati yake hekta 30,802 zinalimwa na kuomba wizara ya kilimo isaidie uanzishwaji wa miradi mingi ya umwagiliaji.
Mkuu huyo wa wilaya alisema sekta ya kilimo imechangia mapato  ya halmashauri kwa asilimia kati ya 25.9 hadi 34 ambapo katika mwaka 2019/20 iliwezesha halmashauri kutoa mikopo ya shilingi milioni 23 kwa vikundi 30 vinavyojishughulisha na kilimo.
Katika hatua nyingine Prof Mkenda ametembelea wakulima wa miwa wa Mtibwa ambapo amepokea kero ya miwa yao kununuliwa Kwa bei chini ya shilingi 63,000 Kwa tani tofauti na ya wakulima wa Kilombero ambao wanauza Kwa shilingi 120,000 Kwa tani.
Akijibu madai hayo Prof Mkenda alieleza kuwa suluhisho la bei ndogo ya miwa ni kuwa na ushindani mzuri kwa wawekezaji zaidi kuanzisha viwanda vidogo vya sukari hali itakayopunguza utegemezi wa wenye viwanda wakubwa .
” Hapa Mtibwa wakulima wengi naambiwa wamepunguza kulima miwa kutokana na kukata tamaa ya bei  toka kiwanda cha sukari Mtibwa ,nitoe rai Kwa taasisi za kifedha za ndani kama TADB,CDRB,NMB na NBC wayoe mikopo kwa wawekezaji kuanzisha viwanda vya sukari ili miwa ya wakulima ipate soko” alisisitiza Waziri Mkenda.
Prof. Mkenda ametembelea pia kiwanda cha sukari Mtibwa na kuzungumzia na uongozi wa kiwanda ambapo amewataka kuhakikisha wananunua miwa ya wakulima ili wazalishe sukari zaidi ya tani 50,000 za sasa kwa kuwa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 100,000 Kwa mwaka.
Waziri Mkenda amerejea agizo lake la kutaka kuona mikataba ya viwanda vya sukari ili ajue kuna nini na wanapaswa kufanya kitu gani zaidi kulingana na mkataba wa ubinafshaji uliofanywa na Serikali mwaka 1999.
“Ni kweli mazingira ya uwekezaji zamani yalikuwa mabaya kwenye uwekezaji wa viwanda vya sukari lakini sasa serikali ya Awamu ya Tano imeboresha sana hivyo tunataka uzalishaji iongezeke” alisisitiza Waziri Mkenda.
Kuhusu malalamiko ya wakulima kuhusu bei ya miwa ya wakulima ipatiwe ufumbuzi haraka ili mkakati wa kiwanda kuongeza uzalishaji uwe na tija .
Akizungumza kuhusu tatizo la wakulima wa miwa Mtibwa ,Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Alibinius Mgonya alisema kiwanda cha Mtibwa hakijatumia kikamilifu eneo lake ikiwemo skimu za umwagiliaji kuzalisha miwa ya kutosha hatua .
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Japhet  Justine amesema katika kuunga mkono jitihada za Rais Dkt.John Pombe Magufuli wamewekeza katika ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Bagamoyo .
“Kwa ushirikiano na CRBD na Standard Chartered Benki yetu TADB tumewekeza kwenye uzalishaji wa sukari Bagamoyo ili kuhakikisha nchi inaondokana na uagizaji sukari nje” alisema Japhet.
Katibu Mkuu Kilimo Gerald Kusaya pamoja na watendaji wakuu wa Benki ya Maendeleo  ya Kilimo(TADB), Bodi ya Sukari na Mrajis Mkuu wanashiriki ziara hiyo pia.