Muonekano wa Barabara ya Tunduru-Seed Farm kwa kiwango cha Lami yenye
urefu wa Km 1.25 iliyojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Muonekano wa Barabara ya Katibu Tarafa-Ikulu Ndogo kwa kiwango cha Lami
yenye urefu wa Mita 490 iliyojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Muonekano wa Barabara ya Peramiho–Morogoro–Nakahuga kwa kiwango cha
Lami yenye urefu wa Km 7.34 iliyojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na
Mijini (TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Muonekano wa sehemu ya Barabara kwa kiwango cha Lami zenye urefu wa km
12.3 zilizojengwa chini ya Mradi wa Uimarishaji Halmashauri za Miji “Urban Local Government Strengthening Program” (ULGSP) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
****************************************
Bebi Kapenya na Thereza Chimagu
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), unaendelea kufanya
matengenezo na maboresho ya miundombinu ya barabara, madaraja na vivuko
katika Mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuifanya miundombinu hiyo iwe
katika hali nzuri kwa kipindi chote cha mwaka kwa lengo la kuwezesha wananchi
kusafiri na kusafirisha bidhaa na mazao yao kwa haraka na kwa gharama nafuu.
Katika Mkoa wa Ruvuma ambao Makala hii inauangazia, TARURA imekuwa
ikihakikisha miundombinu ya barabara hasa mashambani inapitika ili kurahisisha
usafirishaji wa mazao ya wakulima yanafika sokoni haraka kwa lengo la kuinua
uchumi wa wananchi.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Mratibu wa TARURA Mkoa wa Ruvuma,
Mhandisi Edward Lemelo anaeleza kuwa tangu TARURA ianzishwe hali ya
barabara katika Mkoa wa Ruvuma asilimia 30 ya mtandao wa barabara una hali
nzuri na hali ya wastani ambapo zinapitika mwaka mzima.
“Tumefanya matengenezo mengi kwa maana ya matengenezo ya Kawaida
(Routine Maintenance) zaidi ya Km 1291.7, matengenezo ya Sehemu Korofi
(Spot Improvement) sehemu zilizokuwa zinasumbua wananchi zaidi ya Km 540,
tumefanya matengenezo ya Muda Maalum yaani matengenezo makubwa
(Periodic Maintenance) zaidi ya Km 665 pamoja na kujenga madaraja madogo na
makalavati 633 katika barabara mbalimbali za TARURA kwenye Mkoa wetu”,
anasema Mhandisi Lemelo.
Mhandisi Lemelo anaeleza kuwa TARURA Mkoa wa Ruvuma imetekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo ambayo kwa kuanzia Halmashauri ya Wilaya ya
Tunduru, Wakala umejenga Daraja kubwa la Fundimbanga lenye urefu wa mita
45 kwa kutumia Shilingi Bilioni 1.5 na sasa wananchi wa eneo hilo wanapita bila
shida tofauti na hapo awali.
“Ukitoka kwenye barabara kubwa kuna kijiji kinaitwa Tabora mpaka kufika kijiji
cha Fundimbanga wananchi walikuwa hawawezi kutoka kwenye vijiji hivyo kufika
mjini hasa kipindi cha masika, lakini tumewezesha wananchi kufikia barabara
kubwa kwa kutumia daraja hilo ili waweze kusafirisha mazao yao kwa urahisi na
kupeleka sokoni”, anasema Mratibu.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ambayo ni
Halmashauri mpya, eneo hilo halikuwahi kuwa na lami lakini kwa kutumia fedha
za Ahadi za Viongozi wamejenga Barabara ya Madaba-LITA Km 1 kwa kiwango
cha Lami na kuweka taa za barabarani. Pia kwa kutumia fedha za Mfuko wa
Barabara wamejenga Barabara ya Kona Bar-NMB-Makalavati Juu kwa kiwango cha Lami yenye urefu wa Mita 750. Pia, wanaendelea na ujenzi wa Barabara ya
Wino-Ifinga-Luhuji kwa kiwango cha Changarawe Km 15 ambapo ikikamilika
itasaidia wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi kwani eneo hilo wanalima
sana mazao ya maharage, mahindi, ndizi, mpunga na tangawizi.
Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, utekelezaji wa miradi
mbalimbali umefanyika ikiwemo ujenzi wa Barabara ya Peramiho-Lundusi Km
6.43 na Peramiho-Morogoro Km 7.34 zote kwa kiwango cha Lami, barabara hizo
zimesaidia wananchi kutoka katika vijiji vya Morogoro na Peramiho kuweza
kufikia hospitali ya Peramiho kwa urahisi zaidi, na kwa sasa wapo katika
maandalizi ya ujenzi wa Daraja la Mto Muhukulu mradi ambao bado upo katika
hatua ya Usanifu (Design) na ujenzi unatarajia kuanza hivi karibuni.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea wamejenga barabara kwa kiwango
cha Lami Km 12.3 na kuweka taa za barabarani kwa kutumia Mradi wa
Uimarishaji Halmashauri za Miji “Urban Local Government Strengthening
Program” (ULGSP) mradi ambao umeweza kupendezesha Mji wa Songea, lakini
pia kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara wamejenga Barabara ya Lami
(Tunduru Seedfarm) Km 0.75, Barabara ya Pachanne-Mjimwema kwa kiwango
cha Lami nyepesi Km 0.4 na Barabara ya Seedfarm kwa kiwango cha
Changarawe Km 3 na pia wanaendelea kujenga Km 1 za Lami kila mwaka ili
kuuboresha Mji.
Mhandisi Lemelo anasema kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga,
wameweza kujenga Barabara ya Mbinga-Litoho kwa kiwango cha Lami Km 25
ambayo hapo awali ilikuwa na hali mbaya kwani wananchi walikuwa
wanatembea wiki nzima kusafirisha mazao yao.
“Kuna sehemu inaitwa Litoho ambapo ni mpakani mwa Nyasa na Mbinga kule
kuna wananchi wengi ambao ni wakulima wa mazao ya kahawa na ndizi
walikuwa wanatumia wiki moja kuleta mazao yao mjini lakini baada ya kuweka
Lami kwa sasa wanatumia dakika 30 tu kufika mjini na kuuza mazao yao kwa
urahisi, kwa hiyo ujenzi wa barabara hii umesaidia sana wakulima kusafirisha
mazao yao kwa urahisi na kwa gharama nafuu”, anasema Mratibu.
Pia katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, wameweza kujenga Daraja kubwa la
Tingi-Lulimbo-Mtuha na kufungua barabara Km 15 katika Barabara ya Tingi-
Lulimbo-Mtuha ambayo imeweza kusaidia wananchi kuvuka kutoka Nyasa
kwenda Wilaya ya Mbinga kwa kutumia njia fupi na kusafirisha mazao yao kwa
haraka kupeleka sokoni, pia kwa kutumia fedha za Ahadi za Viongozi
wametengeneza Lami Km 1 na kuweka taa za barabarani kwa lengo la
kuuboresha Mji.
Aidha, wamejenga Barabara ya Tumbi-Mango-Kindili kwa kutumia zege (concrete
strips) Km 15 sehemu ambayo ilikuwa korofi lakini baada ya ujenzi wa barabara
hiyo imewasaidia wananchi kuzifikia huduma za afya kwa urahisi.
TARURA katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga kazi kubwa iliyofanyika ni
matengenezo ya barabara ya Lipembe yenye urefu wa Km 32.61 kwa kiwango
cha Changarawe ambapo hapo awali ilikuwa haipitiki lakini baada ya
matengenezo hayo imeweza kusaidia wananchi katika suala la usafiri. Pia,
wamejenga Barabara ya Mpepai-Kihungu Km 16.50 na Pachasita-Tulila Km 10.66
kwa kiwango cha lami.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo wameboresha Barabara iitwayo
Libango–Kiburungutu-Mtumbatimaji kwa kiwango cha Changarawe Km 10
barabara ambayo inatoka katika kijiji cha Libango kuja mjini sehemu ambayo
kuna wakulima wa mazao ya mahindi na ufuta na kusaidia wananchi hao
kuvusha mazao yao kutoka mashambani hadi mjini kwenye masoko.
Mkazi wa Kijiji cha Fundimbanga Wilaya ya Tunduru Bw. Alto Luambano,
anaipongeza TARURA kwa kutengeneza Daraja kubwa la Fundimbanga lenye
Mita 45 ambalo limesaidia kusafirisha mazao na hivyo kufika sokoni kwa urahisi.
“Kabla ya ujenzi wa daraja hili, wananchi wa vijiji vya Tabora na Fundimbanga
tulipata shida katika kusafirisha mazao yetu lakini TARURA wametuondolea hilo
tatizo kwa kututengenezea daraja ili tuweze kufika barabara kubwa na
kusafirisha mazao yetu kwa urahisi na kupeleka sokoni”, anasema Bw.
Luambano.
Naye, Jeremiah Makelele ambaye ni mkulima wa zao la maharage Kata ya Wino
Halmashauri ya Madaba, anasema katika Kata yao wanalima sana mazao ya
maharage, mahindi, ndizi, mpunga, tangawizi pamoja na uvunaji wa mazao ya
misitu, vilevile eneo hilo lina shughuli za kijamii kama vile shule na vituo vya
afya, hivyo mahitaji ya miundombinu bora na ya uhakika ni muhimu sana na
anaipongeza TARURA kwa kuanza ujenzi wa Barabara ya Wino-Ifinga-Luhuji
yenye urefu wa Km 15 kwa kiwango cha Changarawe ambayo itawasaidia
kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
Naye, Bi. Happy Sawali Mkazi wa Peramiho Wilaya ya Songea, anaipongeza
Serikali kupitia TARURA kwa kutengeneza ya Barabara ya Peramiho-Lundusi Km
6.43 na Peramiho-Morogoro Km 7.34 zote kwa kiwango cha Lami na kwamba
barabara hizo zimerahisisha usafiri na kusaidia wananchi kutoka katika vijiji vya
Morogoro na Peramiho kufikia hospitali ya Peramiho kwa urahisi.
Kwa upande wake Bw. Othman Ndunguru, Mkazi wa Kijiji cha Matutu Wilaya ya
Mbinga, anasema anawashukuru TARURA kwa kujenga Barabara ya Mbinga- Litoho kwa kiwango cha Lami Km 25 kwani barabara hiyo ni muhimu kwavile
inaunganisha Wilaya ya Nyasa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
“Barabara hii inatupunguzia umbali mrefu sisi wananchi ambao tulikuwa
tunalazimika kuzunguka umbali mrefu kwenda Mbinga ambapo tulikuwa
tunatumia wiki moja, lakini baada ya ujenzi wa barabara hii tunatumia dakika 30
tu kufika Mbinga, hivyo tunaishukuru sana TARURA kwa kututengenezea
barabara hii na sasa tunasafirisha mazao yetu kwa urahisi”, anasema Bw.
Ndunguru.
Mkoa wa Ruvuma una mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa Km
7,143.7 ambao unahudumiwa na TARURA na kati ya hizo jumla ya Km 82.2 ni
Barabara za Lami ambazo ni asilimia 1.2% ya mtandao mzima, jumla ya Km 937
ni Barabara za Changarawe ambazo ni asilimia 11.7% ya mtandao mzima na
jumla ya Km 6,124.5 ni Barabara za Udongo ambazo ni asilimia 87.1% ya
mtandao mzima.