Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Waitara akizungumza na wawakilishi wa viongozi kutoka Wilaya ya Nzega mkoani Tabora na maafisa mazingira (hawapo pichani) kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nzega alipofanya ziara mkoani humo kwa ajili ya kuhimiza uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Waitara akisamiliana na wawakilishi wa viongozi kutoka Wilaya ya Nzega mkoani Tabora na maafisa mazingira kutoka Wilaya ya Nzega mkoani Tabora alipofanya ziara mkoani humo kwa ajili ya kuhimiza uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira yam waka 2004.
*****************************************
Halmashauri zote nchi zimetakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za kuhifadhi na kusimamia mazingira katika maeneo yao.
Agizo hilo limetolewa leo na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Waitara kwa nyakati tofauti alipofanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mji na Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Akiwa katika ziara hiyo Waitara alisema kuwa kwa kutenga fedha hizo kutazisaidia halmashauri hizo kuweza kupata vitendea kazi vitakavyotumika katika usafi wa mazingira.
“Huwezi kusema unazoa taka wakati huna hata vitenfdea kazi kwa hiyo halmashauri zinapaswa kutenga asilimia kumi ya bajeti zao kwa mwaka na kuweka mikakati ya kutunza mazingira,” alisema.
Aidha alitoa wito kwa halmashauri zote kuhakikisha vinaundwa vikundi vitakavyojishusisha na uzoaji taka mitaani ili kuweka maeneo yao katika hali ya usafi.
Naibu Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kuipongeza Halmashauri ya Nzega kwa kuwa na kulipa kipaumbele suala la mazingira ambapo kwa sasa kupitia mapato yao ya ndani wametenga ferdha kwa ajili ya kununua gari la kukusanya na kusafirisha taka.
Pia aliipongeza Nzega kutekeleza agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuzitaka kila halmashauri kupanda miti milioni moja.