Home Mchanganyiko CHUO KIKUU HURIA KUJENGA MAABARA SABA ZA KISAYANSI

CHUO KIKUU HURIA KUJENGA MAABARA SABA ZA KISAYANSI

0

…………………………………………………………………………………..

NA VICTOR MAKINDA. MOROGORO

Chuo Kikuu  Huria cha Tanzania (OUT) kinatarajia kujenga maabara saba za kisayansi kwa ajili ya kukuza ufanisi wa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi katika chuo hicho.

 Hayo yalisemwa  mjini Morogoro jana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Profesa Elifas Bisanda kwenye mkutano wa saba wa  baraza kuu la saba la wafanyakazi wa chuo hicho.

 Profesa Bisanda alisema kuwa tayari wameandika andiko Benki ya Dunia (WB), andiko ambalo  limekubaliwa na wanatarajia kujenga maabara saba katika kanda saba ambazo ni kanda ya Kusini, kaskazini,  nyanda za juu kusini, kanda ya ziwa, kanda ya kati, kanda ya magharibi  na kanda ya pwani.

“Katika maabara hizo kutakuwa na maabara za masomo yote ya sayansi  ambayo ni  Fizikia, Kemia, Bailojia na Tehama, lakini pia tutaweka maabara za lishe na chakula ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi wanaosoma masomo ya lishe na chakula.” Alisema Profesa Bisanda.

 Profesa Bisanda aliongeza kusema kuwa kwa sasa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, wanafanya majaribio yao ya kisayansi ya vitendo kwenye   maabara zilizopo katika vyuo vikuu vingine nchini.

Kuhusu maendeleo ya chuo hicho, Profesa Bisanda alisema  kuwa katika mwaka wa fedha uliopita walipata fedha kiasi cha Shilingi Bil 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitano vya chuo hicho, ambavyo ni Simiyu, Kigoma,Lindi, Manyara na Geita. Alisema kuwa ujenzi wa vituo hivyo umefikia asilimia 90 na wanatarajia kukamilisha ujenzi huo mwezi Mei mwaka huu.  

 Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza hilo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare alisema kuwa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania kina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi  hasa katika kuwasaidia wananchi kuzalisha  mazao bora ya kilimo hivyo aliwaasa wana taaluma wa chuo hicho kuendelea kufanya tafiti za kina kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi na kuchocheza uzalishaji wa mazao ya kilimo. 

Naye Dkt. Wambuka Rangi, Mkurugenzi wa Kituo cha Morogoro, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,(OUT) alisema kuwa Chuo hicho ni mahali  sahihi pa kupata elimu bora kuanzia ngazi ya cheti mpaka Uzamivu (PHD) kwa njia ya masafa (online), hivyo mtu yeyote mahali popote alipo anaweza kusoma pasipo kuathiri shughuli zake za kawaida za kila siku.

Akizungumzia kuhusu mkutano wa saba wa baraza  la wafanyakazi wa chuo kikuu huria, Dkt Wambuka alisema baraza hilo ni mahususi kwa ajili ya kujadili maslahi ya wafanyakazi na namna ya kuboresa huduma.

“ Tunachotegemea baada ya baraza hili ni  kutoka na mikakati mbali mbali ambayo itahitaji utekelezaji kwa ajili ya matokea chanya ambayo yataongeza tija, kuboresha huduma na masalahi. Alisema Dkt Wambuka.