Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Burilo Deya akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Siasa Wilaya ya Busega, kamati hiyo ilipotembelea Shule ya Msingi Irambo kujionea utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu shuleni hapo.
……………………………………………………………………………………
Kamati ya Siasa Wilaya ya Busega imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa. Kamati hiyo ilifanya ziara ya siku mbili kati ya tarehe 12 hadi 13 Februari 2021 ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa.
Kamati hiyo iliweza kutembelea miradi 8 na kujionea jinsi utekelezaji wake unavyoendelea. Pamoja na kujionea utekelezaji wa miradi hiyo kamati imetaka kutatuliwa haraka changamoto zinazoathiri ukamilikaji wa miradi kwa wakati.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Daudi Ng’ondi amesema kwamba anawashukuru watumishi wa Wilaya ya Busega kwani wanaofanya kazi kwa kujituma na anawataka waendelee kufanya kazi kwa kujitoa ili kufikia lengo la Serikali.
Aidha, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Burilo Deya amesema changamoto zote zillizojitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo zitafanyiwa kazi na ameitoa hofu kamati hiyo, huku akieleza kwamba utekezaji wa miradi mbalimbali unakwenda vizuri kama kamati ilivyoweza kutembelea licha ya changamoto ndogondogo.
Kamati hiyo iliweza kutembelea miradi ya ujenzi wa miundombinu kwenye Shule ya Sekondari Antony Mtaka, ambapo kamati iliweza kujionea miundombinu ya ujenzi wa Bwalo, Maabara, Madarasa na Vyoo kwa thamani ya TZS Milioni 196.6.
miradi mingine iliyotembelewa na kamati hiyo ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Sekondari Venance Mabeyo na kujionea ujenzi wa Maabara, Madarasa na Vyoo kwa thamani ya TZS Milioni 46.3, Shule ya msingi Irambo ambapo utekelezaji wa ujenzi wa madarasa na vyoo kwa thamani ya TZS Milioni 66.6, ujenzi Jengo la Utawala Wilaya ya Busega ambalo linagharamu zaidi ya TZS bilioni 4.9 ambapo limeanza kutumika huku vyumba 68 vikiwa vimekalika kati ya vyumba 97 na ujenzi wake unaendelea.
Aidha kamati hiyo iliweza kutembelea ujenzi wa Jengo la Uthibiti Ubora wa Shule, ambapo ujenzi wake unagharimu zaidi ya TZS Milioni181.1, upanuzi wa wodi ya wazazi katika Zahanati ya Mwamagigisi na ujenzi wa Jengo la Rafiki kwa Vijana (Youth Friendly Corner) ambapo ujenzi wake ni TZS Milioni 33. Kwa upande mwingine kamati iliweza kutembelea miundombinu ya barabara kata ya Lamadi na kumpongeza meneja wa TARURA Mhandisi Mwita Muhochi kwa jitihada anazozifanya kuhakikisha barabara zinapitika lakini kamati imemtaka kuongeza nguvu ya ujenzi wa barabara maeneo mbalimbali wilayani Busega ikiwemo zilizomo kwenye kata hiyo. . Kamati pia iliweza kutembelea kikundi cha Wanawake kijulikanacho kama Umoja ambacho kimepatiwa mkopo wa TZS Milioni 3.5, fedha zinazotokana na mapato ya ndani kutoka Halmashauri ya wilaya ya Busega. kikundi hicho kinachopatikana kata ya Nyashimo kinajuhusisha na ufugaji wa Mbuzi.
Awali Mhe. Ng’ondi amesisitiza kwamba utekelezaji wa miradi hasa wa ujenzi wa majengo unahitaji umakini ili kuwa na uimara wa majengo hayo. “Tunahitaji kuwa na majengo bora na sio bora majengo” aliongeza Mhe. Ng’ondi. Hata hivyo kamati hiyo imewataka watumishi wilayani Busega kufanya kazi kwa kujitoa, lakini imetoa pongeza kwa Mhandisi wa majengo Wilaya ya Busega Bw. Paul Tumbu kwa kusimamia vyema ujenzi wa miundombinu mbalimbali.