……………………………………………………………………
Naibu Waziri Wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega ametoa ushauri kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuona namna ya kuzishauri Taasisi za Fedha nchini kutumia lugha ya kiswahili katika huduma mbalimbali kwa wateja wao.
Naibu Waziri Mhe. Ulega ametoa ushauri huo Februari 12, 2021 mara baada ya kukutana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florence Luoga ambapo amesema huduma za kifedha nchini zinatolewa kwa lugha ya Kingereza ambayo wengi hawaielewi ipasavyo.
“Kwenye eneo la Huduma za kifedha hasa katika mikataba lugha inayotumika ni kiingereza, hivyo sisi Serikali tumeona ipo haja kushauriana na nyie kuona namna ambavyo tunaweza kuyashauri mabenki kutumia lugha ya kiswahili kwa wateja wao ambao ni watanzania” alisema Mhe.Ulega.
Mhe. Ulega ameongeza kuwa Wizara yake ina wataalam katika lugha hiyo ambao wanapatikana Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), hivyo kama Benki zitahitaji wataalamu wa kutafsiri mikataba pamoja na huduma nyingine, Baraza hilo lipo tayari kutoa ushirikiano.
Kwa upande wake Gavana wa BoT, Prof. Luoga amesema, amepokea mawazo ya Serikali na ofisi yake itayafanyia kazi, huku akieleza kuwa Benki hiyo ipo katika mchakato wa kuhakikisha Watanzania wanatumia huduma za kibenki, hivyo ushauri huo utasaidia kufanikisha azma ya benki hiyo.
“Kila mtanzania ana haki ya kupata huduma za kibenki kwa urahisi, chagamoto iliyopo ni lugha inayotumika hasa katika mikataba, hivyo wazo la kitumia lugha yetu ya kiswahili ni jema na litasaidia kupata wateja wengi zaidi” alisema Prof. Luoga.
Prof. Luoga ameongeza kuwa matumizi ya lugha ya kiswahili yatasaidia kuhamasisha wananchi wengi zaidi kutumia huduma za kibenki, huku akisisitiza pindi itakopanza kutekeleza ushauri huo, ushiriki Wa BAKITA ni muhimu katika kutafsiri kwa usahihi na kuleta maana ambayo imekusudiwa.