……………………………………………………………………………………………
Na Shamimu Nyaki – WHUSM, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Hassan Abbasi amewashukuru wananchi wa Dodoma na watanzania wote kwa namna ambavyo wamefanikisha Tamasha la Serengeti Music Festival Dodoma lililofanyika Februari 06, 2021 Uwanja wa Jamhuri jijini hapo.
Dkt Abbasi ametoa Shukrani hizo kwa njia ya Video Februari 12, 2021 jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa wakati wananchi wanatimiza wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli wa kufanya kazi, lakini Wizara yake inayo sekta ya kuhakikisha wananchi baada ya kufanya kazi wanapata burudani.
“Nawapongeza na kuwashukuru wadau wote waliofanikisha Tamasha la Serengeti Music Festival, tumefanya kazi kubwa na kuionesha Afrika na Dunia kwa ujumla kuwa Tanzania ya kipato cha kati ambayo ni ya kazi zaidi lakini pia burudani ndio sehemu yake”, alisema Dkt.Abbasi.
Akiendelea kuzungumza katika salamu hizo, Dkt Abbasi amewashukuru wanadodoma kwa jinsi walivyokuwa na ari ya kupata burudani licha ya kuloa na mvua iliyokuwa inanyesha siku hiyo,hali iliyolazimu wasanii kuendelea kutoa burudani kwa hadhira hiyo.
“Kila nikiangalia picha za siku ile kama Kiongozi wa Sekta hii na msimamizi wa Tamasha nasema Dodoma hatuwezi kuwaacha tutarejea tena”, alisisitiza Dkt.Abbasi.
Aidha, Dkt Abbasi amewashukuru wasanii, wadhamini, viongozi wa Serikali, wabunge wakiongozwa na Naibu Spika, Mhe. Tulia Akson wafanyakazi wa Wizara yake, washereheshaji, madjs, serikali ya wanafunzi, wanafunzi pamoja na watanzania wote kwa ujumla.