…………………………………………………………………………………….
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Mjini kimefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Hombolo Makulu, Mkapa na Sekondari za Kikombo na Hombolo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa na Sekretarieti ya Chama hicho, Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma, Diana Madukwa amesema wamefurahishwa na namna ujenzi huo unavyoenda kwa kasi huku akisema kukamilika kwa madarasa hayo kutasaidia kuchangia ukuaji wa elimu kwenye shule hizo.
Kamati hiyo ya siasa imeuagiza uongozi wa shule hizo kuhakikisha ujenzi wa shule hizo unakamilika kwa wakati huku wakisema agizo hilo siyo kwa shule hizo tu bali shule zote za Jiji la Dodoma ambazo zinaendelea na ujenzi wa miundombinu yake.
” Niwapongeze sana ndugu zetu Walimu wote wa Shule za Msingi na Sekondari kwa namna mnavyojituma katika kufundisha wanafunzi, niwahimize tu kuhakikisha mnazingatia utunzaji wa mazingira yenu ya shule ikiwemo usafi wa choo.
Kamati ya Siasa ya Wilaya pia imefurahishwa na maendeleo ya ujenzi hasa katika Sekondari ya Kikombo ambayo ni miongoni mwa shule za Jiji letu zilizofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne,” Amesema Diana Madukwa.
Kamati hiyo ya siasa chini ya Mwenyekiti wake, Johnick Risasi inafanya ziara ya wiki nzima kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ndani ya Jiji la Dodoma ikiwemo ile ya Afya, Elimu, Miundombinu ya Barabara na Maji.