Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Utendaji ya Mkurabita, Immaculata Senje (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wanufaika wa Mkurabita waliokabidhiwa Hatimiliki za kumiliki ardhi Shehia ya Welezo, Wilaya ya Magharibi A, Unguja Zanzibar Februari 9,2021. PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Utendaji ya Mkurabita, Immaculata Senje (kushoto), akimkabidhi hatimiliki Said Mbarouk Rajab.
Senje akimkabidhi hatimiliki Ghashima Juma Salum
Senje akimkabidhi hatimiliki Sheha wa Shehia ya Welezo, Mohamed Amour Khamis
|
Moja ya mfano wa hatimiliki walizokabidhiwa wakaazi wa Shehia ya Welezo. |
Wakaazi wa Shehia ya Welezo wakikabidhiwa hatimiliki za kumiliki Ardhi
Afisa Sheria Benki ya Watu Zanzibar (PBZ), Ali Alhaj Masoud akihamasisha wanufaika wa Mkurabita waliokabidhiwa hatimiliki za ardhi katika Shehia ya Welezo kuzitumia hati hizo kwenye benki hiyo kuomba mikopo .
Afisa Mahusiano wa Amana Bank Tawi la Zanzibar, Anuar Rashid Said akitoa mafunzo jinsi ya kuzitumia hati hizo kukopa benki kwa masharti nafuu.
Msimamizi wa Mikopo wa Amana Bank Zanzibar, Abdalah Mtunguja akitoa ufafanuzi wa masharti ya benki baada ya mmoja wa wakaazi wa Welezo aliyekabidhiwa hatimiliki.
Sehemu ya wakaazi wa Shehia ya Welezo wakiwa katika mkutano huo.
Afisa Ushirika wa Wilaya ya Magharibi A, Hassan Ali Mbarouk akielezea jinsi ofisi yake inavyosaidia wakaazi kusajiri ardhi na mali zao zingine kupata hatimiliki.
Mrajis wa Ardhi Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar Abdul Nasser Hikimany akielezea umuhimu na faida za hatimiliki walizokabidhiwa.
Afisa Mrasimishaji (Mtambuzi) wa Ardhi Unguja, Shawana Said Khamis akielezea utaratibu wa kupata haimiliki hizo.
Mratibu wa Mkurabita, Dkt. Serphia Mgembe akitoa neno la utangulizi wakati wa shughuli ya kukabidhi hatimiliki.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Utendaji ya Mkurabita, Immaculata Senje akizungumza wakati wa kukabidhi hatimiliki ambapo aliwaasa kuzitumia kukopa fedha benki badala ya kuzifungia kabatini.
Wanufaika wakiwa na furaha baada ya kukabidhiwa hatimliki hizo.
Na Richard Mwaikenda, Zanzibar
WANUFAIKA 50 wa Mpango wa Kurasimisha Ardhi na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), wamekabidhiwa Hati za Hakimiliki katika Shehia ya Welezo, Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.
Hati hizo zinazoandaliwa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, zimekabidhiwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Utendaji ya Mkurabita, Immaculata Senje katika hafla iliyofanyika leo Februari 9,2021 shehia ya Welezo, wilaya ya Magharibi A.
Kabla ya kukabidhiwa hati hizo, wanufaika walipata mafunzo ya jinsi ya kuzitumia hati hizo kama dhamana kukopa fedha Benki na taasisi zingine za fedha kwa ajili ya kuinua biashara zao hivyo kunufaika kimaisha.
Wananchi hao walipigwa msasa na maofisa wa baadhi ya benki na maafisa wa serikali kwa kuwaeleza kuwa hati hizo zina thamani kubwa hivyo wazitunze vizuri na kuzitumia kukopa kwenye benki zao badala ya kuzifungia kabatini.
Maofisa waliotoa mafunzo ni Afisa Sheria Benki ya Watu Zanzibar (PBZ), Ali Alhaj Masoud, Afisa Mahusiano wa Amana Bank Tawi la Zanzibar, Anuar Rashid Said, Msimamizi wa Mikopo wa Amana Bank Zanzibar, Abdalah Mtunguja na Afisa Ushirika wa Wilaya ya Magharibi A, Hassan Ali Mbarouk.
Awali kabla ya kukabidhi vyeti, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mkurabita, Immaculata Senje amesema kuwa katika moja ya hotuba za Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi alitaja moja ya vipaumbele vyake katika uongozi wake kuwa ni urasimishaji wa ardhi itakayopelekea kupunguza migogoro ya ardhi, hivyo wananchi wanatakiwa kumsaidia Rais kwa kujitokeza kwa wingi kurasimisha ardhi zao.
Amesema ardhi inayorasimishwa inatoka kwenye mtaji mfu kuwa mtaji hai, hivyo hati walizokabidhiwa wazitumie kukopea fedha benki zitakazowasaidia , kujikwamua kimaisha.
“Jambo tulilozindua leo si jambo dogo ni jambo kubwa na tungetamani lienee katika kila eneo, na utaratibu huu tuliofanya leo wa kutoa elimu ya utoaji hati tutaendelea nao,kila mahali tutakapozitoa mara tutaendelea kuwapa faida ya hati hizo. ili ifikie lengo la mkurabita la wananchi kujikwamua kiuchumi, kuondokana na hali ya umasikini kuingia kwenye uchumi mzuri,” amesema Senje.
Ametoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kumuunga mkono Rais kumalizana na migogoro ya ardhi,kupandisha thamani ya ardhi, inakuwa tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kupimwa na kuwataka waliopata hati wawe walimu kwa wengine.
Mratibu wa Mkurabita, Dkt. Seraphia Mgembe aliwapongeza maafisa wa benki waliotoa mafunzo lakini vilevile aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika hafla hiyo.
“Kila mmoja ajipange vizuri apange kuwa atafanya jambo lake la kufanya kwa kutumia hati hizo kukopea fedha benki na kwamba fursa waliyoipata waitumie kwa ukamilifu,” amesema Dkt Mgembe.
Aliziomba benki zitakazofaidika kwa wanufaika wa Mkurabita waliopata hatimiliki kukopa kwao zisaidie kutoa msaada wa kifedha wa kukamilisha mchakato wa kuwapatia hati wananchi katika maeneo ambayo hawajapata bado.