Mlengwa wa Mpango wa kunusuru kaya masikini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) kutoka Kijiji cha Mbuyuni wilayani Uyui, Mkoani Tabora Zainabu Msabila akiwaonyesha jana waandishi wa habari (hawapo katika picha) baadhi ya mbuzi zake ambazo ni matokeo ya fedha za TASAF .
Mlengwa wa Mpango wa kunusuru kaya masikini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) Kijiji cha Mbuyuni Kata ya Kigwa wilayani Uyui Asha Msabila akiwa jana katika shamba lenye ukubwa wa ekari mmoja ambalo alilikodisha kwa fedha zinazotokana na Mpango wa kunusuru kaya masikini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) na kulima mahindi.
Mkazi wa Kijiji cha Mbuyuni Kata ya Kigwa wilayani Uyui Asha Msabila akiwaonyesha jana waandishi wa habari (hawapo katika picha) mahindi katika shamba lenye ukubwa wa ekari mmoja ambalo alilikodisha kwa fedha zinazotokana na Mpango wa kunusuru kaya masikini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) na kulima mahindi.
…………………………………………………………………………………………..
NA TIGANYA VINCENT
WALENGWA wa Mpango wa kunusuru kaya masikini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) wilayani Uyui, Mkoani Tabora wameiomba Serikali kuwawezesha kupata maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
Hatua hiyo inatokana na walengwa wengi kutokuwa na mashamba na hivyo kulazamika kukodisha kwa gharama ya shilingi 30,000/= kwa kila ekari mmoja.
Walengwa hao walitoa kauli hiyo jana wakati ziara ya Waandishi wa habari waliongozana na Viongozi kutoka TASAF Makao makuu iliyolenga kuangalia mafanikio mbalimbali walipata kutokana na fedha wanazopatiwa kila baada ya miezi miwili.
Mkazi wa Kijiji cha Mbuyuni Kata ya Kigwa wilayani Uyui Asha Msabila alisema amelima ekari mmoja ya mahindi kwa sababu ya kukosa eneo na hivyo kutumia fedha anayopatiwa kukodi shamba badala ya kununulia pembejeo ambazo zingemwezesha kulima eneo kubwa na kupata mavuno mengi.
Alisema hivi sasa gharama za ununuzi wa ekari mmoja kwenye kijiji chao unagharimu kuanzia shilingi laki mmoja hadi laki mbili ,jambo ambalo linakuwa gumu kwao.
Asha aliongeza kuwa kwa mwaka huu amekodisha ekari mmoja na kupanda mahindi ambapo anatarajia kuvuna kiasi cha gunia ishiriini na kama engekuwa na mashamba yake angeliweza kulima zaidi ya ekari moja na kupata mavuno mengi.
Naye Marietha Amri alisema ukosefu wa eneo kwa ajili ya kilimo umemsababisha kulima eneo dogo la mahindi ambapo mavuno yake hayawezi kumwezesha kuwa na chakula cha kutosha mwaka mzima.
Aliongeza kuwa wakati mwingine analazimika kukodi eneo kwa ajili ya kulima bustani ya vitunguu ambapo anavuna kiasi cha gunia mbili.
Alisema angekuwa na shamba lake angelima eneo kubwa na kupata mavuno mengi ambayo yangemsaidia kupiga hatua zaidi.
Hata hivyo Mairietha aliishukuru Serikali kwa kuwawezesha kuboresha maisha yao na kuiomba kuwasaidia waweze kumiliki maeneo kwa ajili ya kupanua kilimo ambacho kitawawezesha kujitegemea.
Katika hatua nyingine Walengwa wa TASAF wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwawezesha kuondokana na hali duni na kupiga hatua mbalimbali za kimaendeleo na kuwa na uhakika wa chakula.
Mkazi wa Kijiji cha Mbuyu Salima Rashid alisema baada ya kupata fedha za TASAF alianza ununuzi wa mbuzi wawili ambao wamezaana na kufikia 20 na kununua ng’ombe wanne.
Alisema kuwa baada ya mafanikio hayo anatarajia kuboresha makazi yake kwa kuezeka nyumba yake kwa bati na kuondokana na adha ya kuvujiwa na maji wakati wa mvua.
Naye Zainabu Msabila mama wa watoto tisa alisema kuwa fedha za TASAF zimemsaidia kupiga hatua ambapo ameweza kununua mbuzi wawili ambao wamezaana na kufikia 22 na kuku kutoka wawili hadi 29.
Alisema fedha hizo pia zimemsaidia kusomesha watoto wake ambapo wawili waweza kufikia ngazi ya elimu ya Sekondari.
Kwa upande wa Mratibu wa TASAF Wilaya ya Dkt. Kija Maige alisema ombi la Walengwa atalifikisha kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya kuona uwezekano wa kuwasaidia wale wasioweza kununua maeneo ili walau wapatiwe ekari mmoja.
Aidha alisema kuwa wanajitahidi kutembelea walengwa kwa ajili ya kutoa elimu waweze kutumia mifugo kuboresha makazi yao