Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Ramadhani Kapela ( wa pili kutoka kushoto)akichangia maoni jana katika Kikao cha Ushauri ya Tabora.
Picha na Tiganya Vincent
……………………………………………………………………………………………
NA TIGANYA VINCENT,RS TABORA
WAJUMBE wa Kamati ya Ushauri ya Manispaa ya Tabora (DCC) wametakiwa kuweka uzalendo mbele wa kujali maslahi mapana ya maendeleo ya wananchi badala kupenda kulipwa posho.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Erick Kitwala baada ya wajumbe kutoka vyama vya upinzani kuacha kujadili mapendekezo ya bajeti ijayo ya mwaka 2021/22 na kutaka kujua kiwango cha posho ya kikao watakayolipwa.
“Sijawahi kuona wajumbe wanaingia katika kikao … kabla ya kuanza kikao na kumalizika wanadai kujua kiwango cha posho…wajumbe tuendelea na kikao Mkurugenzi Mtendaji amezingatia suala la posho ya wajumbe husika, mpatapewa baada ya kikao” alisisitiza.
Kitwala alisema kikao cha DCC ni muhimu kwa kuwa kinajadili masuala mapana ya kuboresha maisha ya wakazi wa Manispaa ya Tabora kuliko kujali posho zaidi.
Alisema yeye binafsi yuko tayari kuachana na posho yake na kuendelea kujadili na kutoa ushauri utakaoboresha mapendekezo ya bajeti ijayo ili iweze kuchochea maendeleo ya wakazi wa Manispaa ya Tabora.
Akijibu hoja za Wajumbe kutoka vyama vya upinzani. Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora Bosco Nduguru alisema posho ipo na watalipwa kwa kiwango cha shilingi elfu Hamsini(50,000/=) kwa kila mjumbe halali wa kikao.
Awali Wajumbe mbalimbali kutoka vyama vya upinzani walikuwa wakidai walipwe kiasi cha shilingi laki moja na nusu (150,000/=)
Katika hatua nyingine Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Ramadhani Kapela akiwataka Wajumbe wa DCC kuwatia moyo viongozi wa Wilaya na Manispaa kwa juhudi kubwa walizozifanya za kuondoa kero mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wafanyabiashara wa masoko mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maji.