MBUNGE wa Nanyamba(CCM), Abdallah Chikota,akichangia bungeni leo Februari 10,2021 Mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango, bajeti ya serikali na mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2021/22
…………………………………………………………………………………..
Na Alex Sonna, Dodoma
MBUNGE wa Nanyamba(CCM), Abdallah Chikota ameshauri mambo matatu katika zao la korosho ikiwamo kuondolewa kodi na tozo katika vifungashio na mashine za kubangua korosho ili ziingizwe kwa wingi nchini.
Pamoja na hayo, aipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa kazi nzuri inayofanya katika utekelezaji wa Mpango wa pili wa Maendeleo ya nchi.
Akichangia bungeni leo kwenye Mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango, bajeti ya serikali na mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2021/22, Chikota amesema katika mpango huo serikali imetekeleza miradi mingi na ile ambayo haijatekelezwa imeingizwa kwenye Mpango wa tatu yaendelee kutekelezwa.
Ameshauri kuongeza thamani kwenye mazao ya biashara hususani zao la korosho na kwamba ubanguaji ndio njia pekee ya kuhakikisha korosho inapata bei nzuri kwenye soko la dunia.
“Kubangua korosho ni mkakati ambao tumeuanza huko nyuma na lengo la kuweka Export levy ilikuwa ni kuzuia wanunuzi ili wasisafirishe korosho ghafi lakini mpango huo naona kama una dosari,”amesema.
Ameeleza kuwa uwezo wa kubangua korosho nchini kwa viwanda vilivyopo ni tani 70,000 na uzalishaji ni takribani tani 220,000 hivyo korosho nyingi inauzwa ikiwa ghafi.
“Mimi nashauri kwamba tukose fedha kidogo leo ili tupate fedha nyingi baadae, na hii itawezekana kwa kuondoa tozo na kodi wakati wa uingizaji wa mashine za kubangua korosh, wawekezaji wanalalamika kodi ni kubwa ili mashine nyingi ziingizwe,”amesema.
Vilevile, ameshauri kuwekwa vivutio maalum kwa wawekezaji wapya na kushauri kuondolewa kwa kodi na tozo katika vifungashio kutokana na wenye viwanda kulalamika kodi kubwa.
“Faida yake ni kwamba tutapunguza gharama ya uwekezaji na tutapata wawekezaji wengi na wawekezaji wa ndani badala ya kutegemea wa nje na tutapata wabanguaji wadogo,Mheshimiwa Mwenyekiti kiwanda kidogo cha ubanguaji mtaji wake ni kama Sh.milioni 60 na kwa sababu Korosho inalimwa katika mikoa zaidi ya 12 tunaweza tukatumia Halmashauri fedha zetu badala ya kutoa zile fedha za mfuko wa vijana kwa vijana mmoja mmoja,”amesema.
Amebainisha kuwa inawezekana kuanzisha viwanda vidogo vya kubangua korosho na vikaongeza ajira pia kwa wanawake na thamani ya fedha itaonekana.
“Wenzetu wa Vietnam na India wanatumia sana Korosho zetu kuongeza ajira kwao na mipango hii wakiisikia watakuwa na hofu na korosho ghafi hacienda kwao, muda ni sasa tuwekeze kwenye ubanguaji ili kuongeza ajira,”amesema.
Hata hivyo, amesema kama uwekezaji ukifanywa kwenye ubanguaji utaongeza ajira ambapo ajira milioni nane zilizoahidiwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM, robo yake zitatokana na ubanguaji wa korosho.
“Hoja yangu ya pili ni kuhusu mradi wa Mchuchuma na Liganga ukiangalia mipango yetu yote mitatu inaendelea kutajwa wakati umefika tuweke sasa fedha za kutosha mradi utekelezwe pamoja na kwenda sambamba na ujenzi wa reli kutoka Mtwara -Mbababay na ile pacha ya Mchuchuma na Liganga tuwekeze ili tupate fedha za kutosha,”amesema.
Ameongeza “Tuweze kupata fedha za kutosha kuwekeza kwenye reli hii ya kusini basi Bandari ya Mtwara itatumika ipasavyo,tunasafirisha tumbaku pia Malawi Zambia na DRC Congo wanatumia reli yetu.”