…………………………………………………………………….
Dar es Salaam
Masoko endelevu, Uwekezaji na Teknolojia za kuongeza thamani bidhaa katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji vyapewa kipaumbele kwenye Maonesho ya Kilimo (Nanenane) yanayoratibwa na mikoa ya ukanda wa Magharibi wa Tanzania ambayo ni Tabora na Kigoma ambapo kitaifa yanatarajiwa kufanyika Ipuli katika mkoa wa Tabora kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2021.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa mkoa wa Tabora Mhe Dkt Philemon Sengati na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye walipofanya ziara katika Ofisi za TanTrade ili kushirikiana katika uratibu wa Maonesho ya Kilimo (NaneNane).
Mhe Dkt Philemon Sengati amesema kwa mara ya kwanza Maonesho hayo yanafanyika katika ukanda wa Magharibi hivyo, ni fursa kubwa kwa mikoa hiyo kuonesha utajiri katika ardhi ambapo utavutia wawekezaji hususan katika kilimo na mifugo ili kuweza kuongeza thamani ili kuweza kuuza katika masoko ya nje
“Mkoa wa Tabora ni mkoa wenye ardhi kubwa (eneo) ndani ya Tanzania, ina misitu mikubwa na minene, mifugo zaidi ya milioni nne na mkoa wa Kigoma pia ina mifugo ya kutosha, tunayo madini, mbuga za wanyama na maeneo mengine mazuri hivyo kupitia Maonesho hayo tutatumia kutangaza fursa hizo kubwa kwaajili ya watu kuwekeza na kufanya biashara” ameongeza Dkt Sengati
Ameendelea kusema kuwa kupitia Maonesho haya, ni fursa kwa wakulima, taasisi binafsi na za serikali na wadau mbalimbali kuonesha mafanikio yao, bidhaa zao ikiwemo ubunifu katika eneo la sayansi na teknolojia, tafiti katika masuala ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Nae, Mhe Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye ameongeza kwa kusema kuwa mikoa ya ukanda wa Magharibi ni lango la biashara ambapo Tanzania inapakana na nchi ya Demokrasia ya Kongo na Burundi hivyo, anatarajia kuona Maonesho ya Kilimo yanabadilisha maisha ya wakulima, wavuvi na wafugaji kwa kuchangia pato la taifa kwa kuongezewa maarifa, teknolojia nzuri zitazosaidia kuchakata malighafi za bidhaa zao
“Serikali imefanya juhudi kubwa katika kuboresha miundo mbinu ya kusafirisha bidhaa kwa njia ya treni, barabara nyingi zinajengwa kwa kiwango cha lami na sasa serikali inajenga meli ya tani 4000 Kigoma eneo la Kibirizi inayotengenezwa na taasisi ya Marine Services Company Services hii yote itarahasha wananchi kufanya biashara na kuvutia wawekezaji” ameeleza Mhe Andengenye
Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bw Edwin Rutageruka amehitimisha kwa kusema kuwa TanTrade itatoa ushirikiano na Mikoa hiyo katika kuratibu Maonesho ya Kilimo kwa kuanza kuandaa miundo mbinu ya eneo litakalofanyika Maonesho ili kuwe na muonekano wa Maonesho kwa kupanga bidhaa kisekta, pia kutakuwa na mikutano ya kibiashara kwa njia za kidigitali kwa lengo la kutafuta masoko endelevu kwa bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuwaunganisha na Balozi za Tanzania zilizo nje ya Tanzania na kutakuwa na huduma ya kliniki ya biashara zitakazosaidia kutatua changamoto za wafanyabiashara.