…………………………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
MAKAMU Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze ,Bagamoyo Mkoa wa Pwani Ismail Msumi, ametoa wiki mbili kwa viongozi wa Kijiji cha Kimange kumaliza deni la maji, ili wananchi waendelee kupata huduma.
Msumi ametoa kauli hiyo katika mkutano kwenye Kitongoji cha Togo, baada ya mkazi aliyejitambulisha kwa jina la Said Mohamed kuelezea changamoto ya huduma hiyo.
Alisema kwa muda mrefu wanalazimika kutumia maji ya tenki la shule ya sekondari Kimange.
“Katika eneo letu maji yamekatwa kutokana na deni linaloelezwa limesababishwa na aliyekuwa ana simamia kituo cha kuchotea maji, kabla ya kufungwa kwa bomba hilo, ukienda kwenye mabomba mengine kipindi cha mvua maji yanapatikana, kiangazi hayapatikani,” alisema mkazi huyo.
Wakitolea ufafanuzi kuhusiana na kilio hicho, Mwenyekiti wa Kijiji Said Bakar na Mtendaji wake Mariamu Selemani walisema kuwa sababu zinazosababisha kukosekana kwa maji kunatokana na deni, ambapo walikwenda kwenye ofisi za DAWASA Chalinze wakaambiwa wanatakiwa kulipa
“Juhudi mbalimbali tumezichukua ikiwemo aliyekabidhiwa kituo cha kuuzia maji, ambapo alisema changamoto hiyo imetokana na yeye kukumbwa na matatizo ya kifamilia huku akiahidi kulipa deni hilo,” alisema Mwenyekiti huyo.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho alisema kwamba baada ya kupewa agizo la kulipa fedha hizo hajapewa mrejesho kama ameshalipa au la, huku akiahidi kulifanyiakazi suala hilo ili huduma ya maji iendelee kupatikana kwa wananchi.
Baada ya maelezo hayo Msumi akasema anatoa wiki mbili mdaiwa huyo awe amelipa deni hilo, kinyume chake atawawajibisha viongozi wote we Kitongoji na Kijiji.