Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki,akizungumza na kamati ya kudumu ya Bunge,Mifugo,Kilimo na Maji katika kikao chenye lengo la kuwapa uwelewa masuala ya chanjo iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge,Mifugo,Kilimo na Maji Mhe. Christina Ishengoma akizungumza wakati walipokutana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kujadali masuala mbalimbali yanayohusu chanjo pamoja na mwongoza uliozinduliwa na wizara uliofanyika bungeni jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul,akizungumza na kamati ya kudumu ya Bunge,Mifugo,Kilimo na Maji katika kikao chenye lengo la kuwapa uelewa kuhusu masuala ya chanjo iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo,Prof.Elisante Ole Gabriel,akijibu hoja za wabunge wa kamati ya kudumu ya Bunge,Mifugo,Kilimo na Maji wakati Wizara ilipokutana na kamati hiyo kuwapa elimu juu ya uelewa masuala ya chanjo iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dk.Stella Bitanyi,akijibu hoja za wabunge wa kamati ya kudumu ya Bunge,Mifugo,Kilimo na Maji walipokutana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika bungeni jijini Dodoma.
Mbunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Charles Mwijage kutoka Jimbo la Muleba Kaskazini CCM,akisisitiza jambo wakati wa kikao cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyokutana na Kamati ya kudumu ya Bunge, Mifugo, Kilimo na Maji bungeni leo Februari 7,2021 katika ukumbi wa Msekwa Dodoma..
Mbunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe.Steven Kiruswa kutoka Jimbo la Longido CCM,akichangia mada wakati wa kikao cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyokutana na Kamati ya kudumu ya Bunge, Mifugo, Kilimo na Maji bungeni leo Februari 7,2021 katika ukumbi wa Msekwa Dodoma..
Baadhi ya wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakifatilia kikao cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi chenye lengo la kuimarisha huduma za chanjo ya mifugo kilichofanyika leo Februari 7,2021 katika ukumbi wa Msekwa Dodoma..
Sehemu ya watumishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakifatilia kikao cha Wizara na Kamati ya kudumu ya Bunge, Mifugo, Kilimo na Maji kilichofanyika bungeni Dodoma
……………………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekutana na Kamati ya kudumu ya Bunge, Mifugo, Kilimo na Maji kueleza masuala mbalimbali ikiwemo uwepo wa mwongozo wa uchanjaji mifugo, usambazaji na usafirishaji wa chanjo.
Akizungumza leo kuhusu kikao hicho, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, amesema Wizara imeeleza namna ilivyoimarisha huduma za chanjo ya mifugo na kuiomba Kamati hiyo ifuatilie na kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kutambua umuhimu wa kuchanja mifugo.
“Tumepokea michango yao mizuri sana waliyotupa kamati, kazi ya Bunge ni kusimamia na kuishauri serikali, wametushauri kwenye mambo mengi yanayohusu chanjo, kuhusu mwongozo pia wametoa ushauri wao, tumewaomba wanaporudi kwenye majimbo yao wasimamie serikali za mitaa zilizopo kule, ili haya tuliyojadili haya yanatimizwa,”amesema.
Ametoa wito kwa wafugaji kuchanja mifugo yao yote wanayofuga kwa kuwa inasaidia kuboresha afya ya mifugo.
“Tunapochanja tunaboresha afya ya mifugo yetu kwa ng;ombe na mbuzi, hasa mifugo inayoliwa ni msingi sana katika kupata soko la mifugo hiyo kwa kuwa na afya inayoeleweka, nitoe wito wafugaji waone umuhimu wa kuchanja pamoja na kwamba serikali ina sheria na taratibu zake lakini nisingependa kukazia kwenye sheria na kanuni nataka nikazie umuhimu wa kuchanja mifugo yetu, ili iwe na tija,”amesema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul, amesema baada ya kuzinduliwa mwongozo huo Wizara ilitoa maelekezo ufike ngazi za Halmashauri na chama cha wafugaji ili kuwepo na ufanisi kwenye mwongozo huo.
“Bei elekezi imeshatoka na azma ya Wizara tutafika hadi ngazi za chini kupitia vyama vya wafugaji ili kuhakikisha mwananchi haonewi, au hatozwi bei tofauti iliyopo kwenye mwongozo wetu, nitoe rai kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini, zoezi hili la kuchanja mifugo ni endelevu wanaweza kufanya wao na si kutoa kwa makampuni na inaweza kuwa chanjo cha mapato kwao, ”amesema.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof.Elisante Ole Gabriel, ametaja vipaumbele vine vikubwa vilivyopo katika sekta ya mifugo kwasasa kushughulika na afya ya mifugo kwa ujumla, kuhimilisha mifugo, kuboresha miundombinu kama vile majosho na masoko kwa ajili ya mazao ya mifugo.
“Afya ya mifugo ni jambo kubwa, afya ya mnyama ina uhusiano mkubwa na afya ya binadamu, magonjwa wanayougua binadamu asilimia 60 yanatokana na magonjwa yanayohama kutoka kwa mifugo kwenda kwa binadamu, tukiweka mkazo wa kudhibiti afya za wanyama tutaokoa kiasi kikubwa cha fedha takribani Sh.Bilioni 160 zinazotumika na Wizara ya Afya kutibu magonjwa hayo,”amesema.
Amesema Tanzania ni nchi ya pili kwa wingi wa mifugo hivyo wanapaswa kuwa bora na kwamba wataweza kuuzwa kwenye masoko ndani na nje.
“Utendaji wa Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania(TVLA) wanasema wakipata Sh.Bilioni 2.6 wataboresha kazi kubwa wanayofanya, ikiwamo vifaa vya kuboresha maabara yao, na watakuwa na uwezo wa kuzalisha Sh.Bilioni 10, kama Wizara tunahakikisha watumishi waliopo TVLA ni wenye taaluma sahihi,”amesema.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dk.Stella Bitanyi, amesema Wakala huo una majukumu mbalimbali ikiwemo utafiti, utambuzi wa magonjwa ya mifugo na kuhakiki ubora wa mifugo na uzalishaji wa chanjo ya mifugo.
Amesema Wakala hiyo imepata mafanikio makubwa kwa miaka nane kwa kuwafikia wananchi kwa ukaribu na kufungua maabara mpya mbili.
“Tunatarajia kufungua kituo kingine kwa kuigawanya kanda ya ziwa kule Bariadi au kuwa na kituo Musoma, tuna eneo tumepewa Nzega, tutafungua kituo kingine Mbeya kule Tukuyu, tunaendelea ikizingatiwa kwenye Ilani ya uchaguzi kwamba tunatakiwa kuweka kliniki ya mifugo kila wilaya, tuna chanjo pia za mifugo tunaanzisha na sasa tunazalisha chanjo aina sita na chanjo ya saba tunatarajia kuanza kuzalisha mwezi Julai, mwaka huu,”amesema.
Amesema mkakati wa Wakala huo ni kuhakikisha chanjo za magonjwa 13 ya kimkakati chanjo zake zizalishwe nchini na kuimarisha chanjo zinazozalishwa na kuongeza uzalishaji wake.
“Tunaendelea kufanyia kazi malengo ya muda wa kati ambapo tunatarajia kukamilisha chanjo tatu mwezi Juni, ambapo chanjo moja ya homa ya mapafu ya mbuzi, tumezalisha wa majaribio kwa ubora unaotakiwa na uzalishaji kamili utaanza mwezi Machi mwaka huu, ugonjwa wa sotoka tunatarajia tutaanza kuzalisha, pia chanjo ya kichaa cha mbwa tunatarajia kupata mwezi juni kama mnavyojua ni tatizo kubwa sana kwasasa ,”amesema.
Mwisho.