Wajumbe wa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui wakiomba dua jana kabla ya kuanza kikao cha kupitisha mapendekezo ya makisio ya shilingi bilioni 34.2 kwa ajili ya mapato na matumizi ya mwaka ujao wa fedha.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Said Ntahondi akifungua kikao jana ambacho kimepitisha mapendekezo ya makisio ya shilingi bilioni 34.2 kwa ajili ya mapato na matumizi ya mwaka ujao wa fedha.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Uyui Moses Pesha akitoa salamu za Serikali jana wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani ambalo lilipitisha mapendekezo ya makisio ya shilingi bilioni 34.2 kwa ajili ya mapato na matumizi ya mwaka ujao wa fedha.
Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora
……………………………………………………………………………………………..
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui limepitisha mapendekezo ya makisio ya shilingi bilioni 34.2 kwa ajili ya mapato na matumizi ya mwaka ujao wa fedha.
Madiwani hao wamepitisha mapendekezo hayo jana katika kikao cha Baraza la kupitia makisio ya mapato na matumizi ya mwaka ujao wa fedha wa 2021/22.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Said Ntahondi alisema vyanzo vya fedha hizo ni pamoja na mapato ya ndani ya shilingi bilioni ambapo wamelenga kukusanya shilingi bilioni 3 , ruzuku ya Serikali kuu shilingi bilioni 29.6, michango ya wadau wa maendeleo bilioni 1.2 na nguvu za wananchi zitachangia milioni 350.
Alisema vipaumbele katika bajeti ijayo vimejikita katika kuimarisha kilimo kwa kuanzisha mashamba darasa katika Kata 30, kuanzisha mashamba ya vitalu na mashamba ya mikorosho, kuboresha huduma za ugani kwa kununua pikipki 5 kwa Maafisa Ugani ili wawafikie wakulima kirahisi kwa ajili ya kuwapa msaada wa kuboresha huduma zao.
Ntahondi alisema vipambaumbele vingine ni kuboresha huduma ya uongeshaji wa mifugo kwa kujenga majosho manne ya mifugo, kuanzisha mashamba darasa ya malisho ya mifugo katika Taarafa zote tatu za Wilaya ya Uyui na kuboresha miundombinu ya elimu kwa ngazi ya msingi na Sekondari.
Aliongeza vingine ni kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa vijiji 3 , kuanzisha Benki ya Ardhi kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya Wilaya hiyo kwenda kuweka na kupima viwanja 1,000.
Ntahondi alisema kuwa bajeti ijayo pia imekusudia kuboresha ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya Wilaya, Vituo vya Afya na kuendeleza ujenzi wa Zahanati 6 na kununua gari la kubeba wagonjwa.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Hemed Magaro akiwasilisha mapato mapato na matumizi kwa kipndi cha kufikia Desemba mwaka uliopita alisema kuwa walikadiria kukusanya na kutumia shilingi bilioni 32.2 katika mwaka wa fedha uliopita kutoka vyanzo mbalimbali.
Alisema hadi kufikia Desemba , 2020 walikuwa wametumia shilingi bilioni 13.4 ikiwa ni sawa na silimai 43 ya makisio yao.