………………………………………………………………………………….
Katibu Tawala Wilaya ya Busega Bw. Rutagumirwa Rutalemwa ameweza kukutana na kuongea na watumishi umma kwa lengo kuu la kusikiliza changamoto na kero zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Katika ziara ya siku mbili mapema wiki iliyopita Bw. Rutalemwa alipata nafasi ya kukutana na kuongea na watumishi wa kata nne, ambazo ni kata za Lamadi, Kalemela, Mkula na Lutubiga, Bw. Rutalemwa amesema kwamba anajua kwamba katika utekelezaji wa majukumu kama watumishi wa umma changamoto haziwezi kukosekana lakini bila kuonana na watumishi ni vigumu kufanya utatuzi wa changamoto hizo.
Bw. Rutalemwa amesema ni muhimu kusiliza hoja mbalimbali za watumishi pia ni fursa nzuri ya kukumbushana haki na wajibu wa watumishi wa umma. Kwa upande mwingine Bw. Rutalemwa ametoa pongezi kwa watumishi wote wilayani Busega. “Nawapongeza sana kwani mnafanya kazi kwa kujitoa na kwa moyo wa uzalendo, hivyo ningeomba tuendelee kujitoa ili kutimiza azma ya Serikali ya kutoa huduma kwa wananchi”, aliongeza Bw. Rutalemwa.
Katika ziara hiyo Bw. Rutalemwa aliambata na baadhi ya wakuu wa Idara kutoka Ofisi ya Mkurugrnzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, akiwemo Wakuu wa Idara ya Elimu Msingi na Sekondari, Mganga Mkuu wa Wilaya, mwakilishi kutoka Idara ya Utumishi, na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Busega. Aidha watumishi wameweza kutoa baadhi ya changamoto zao zikiwemo changamoto ya uchache wa vifaa vya kutendea kazi, madai ya stahiki zao, na ubovu wa miundombinu kwa baadhi ya maeneo ya vituo vya kazi.
Hata hivyo Bw. Rutalemwa ameweza kuwatoa hofu watumishi, kwamba changamoto hizo zitatatuliwa kwani hata hapo nyuma kulikuwa na changamoto nyingi za watumishi lakini Serikali kwa kuona changamoto hizo imeweza kutatua na mpaka sasa sehemu ya changamoto hizo hazipo tena. Kwa upande mwingine amewataka watumishi wasisite kuwasilisha changamoto zao, kwani Ofisi yake ipo wazi muda wowote. Pia amewaomba watumishi kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na serikali ili kufikia malengo.
Aidha, mwakilishi wa Afisa Utumishi Wilaya ya Busega Bw. Ramadhan Boimanda amewataka watumishi kufuata taratibu za utumishi, ameongea hayo alipokuwa akijibu hoja ya mtumishi aliyetaka kujua ni kwanini hakuna utaratibu wa kuwakilishwa katika uchukuaji na upelekaji wa nyaraka mbalimbali katika Ofisi ya Mkurugenzi ili kuokoa muda na kupunguza gharama. “Tunapenda mtumishi afike ofisini yeye mwenyewe ili kujiridhisha na taarifa zake na sio kumtuma mwakilishi kwani baadhi ya taarifa muhimu hatutaweza kuzipata kwa wakati, hivyo ni vyema mtumishi akafika yeye mwenyewe na nyaraka zake ili tujiridhishe”, aliongeza Bw. Boimanda.
Kwa upande mwingine Bw. Rutalemwa amewataka watumishi kutojiingiza katika masuala yatakayowafanya kupoteza sifa za utumishi ikiwemo kuijiinga katika mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi, kwani hiyo inachafua utumishi wa umma, na kuwataka wao wawe mabalozi wa mapambano ya kuzuia mimba kwa Wanafunzi.
Aidha Bw. Rutalemwa amesema utaratibu wa kukutana na watumishi ni endelevu, hivyo ataendelea kuwatembelea watumishi mara kwa mara, kwani ana imani utaratibu huo una manufaa makubwa kwa watumishi wa umma wilayani Busega.