Na Damian Kunambi, Njombe.
Mlezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Njombe ambaye pia ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa, Dkt. Frank Awasi amewataka wananchi kutumia fursa mbalimbali zilizopo na zitakazojitokeza pindi barabara ya kutoka Lusitu hadiu Mawengi inayojengwa kwa kiwango cha zege yenye urefu wa kilometa 50 utakapokamilika.
Hayo ameyasema katika hitimisho la maadhimisho ya kutimiza miaka 44 ya chama hicho ambayo kimkoa yamefanyika wilayani Ludewa kwa kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali pamoja na mtu mmoja mmoja.
Amesema Ludewa ina fursa nyinyi za kimaendeleo ambayo hukwamishwa kuendelea kutokana na miundombinu mibovu ya barabara hivyo endapo barabara hiyo itaka itakuwa mkombozi kwa wakazi wa Ludewa.
Barabara hiyo inagharimu kiasi cha sh. Bilioni 167.5 mpaka kukamilika kwakwe ambapo kwa sasa tayari km. 26 zimekamilika na kusalia km. 24 ambazo zinatarajiwa kumaliziwa ndani ya mwaka huu barabara ambapo ikikamilika itawawezesha wananchi hao kupata maendeleo kwakuwa miradi mbalimbali itaanza kutekelezwa kama ya Liganga na Mchuchuma.
“Fursa hizi za Liganga na Mchuchuma zitafunguka muda si mrefu na ninyi mtashuhudia kwa macho yenu ya nyama, kwani serikali ya rais John Magufuli ipo kwaajili ya kuhakikisha wananchi wake wanapata Maendeleo kwa kutumia fursa mbalimbali ikiwemo zilizopo katika wilaya zao”, Alisema Dkt.Awasi.
Sanjari na hilo pia Dkt. Awasi alitembelea mradi wa ujenzi wa zahanati unaojengwa katika Kijiji cha Mdilidili kilichopo katika kata ya Lugarawa wilaya humo, shule ya sekondari Lugarawa, chuo cha uuguzi na baada ya hapo alifika katika ofisi ya wilaya ya chama hicho na kuongea na madiwani.
Alipokuwa katika shule ya sekondari Lugarawa alipewa fursa ya kupanda mti wa mparachichi pamoja na baadhi ya viongozi wengine alioongozana nao ambao ni mkuu wa mkoa huo Mhandisi Marwa Rubirya, mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Njombe Jasel Mwamwala pamoja na mjumbe wa halmashauri kuu CCM taifa(MNEC) Fidelis Lumato.
Aidha kwa upande wa mkuu wa mkoa huo Mhandisi Marwa Rubirya aligoma kupanda mti aliokabidhiwa na kudai kuwa atafanya hivyo siku atakoyoenda tena baada kukamilika ujenzi huo wa vyumba vitatu vya madarasa kwani kwa sasa kuna marekebisho ambayo wanatakiwa kuyafanya ikiwemo kuongeza ukubwa wa ubao wa kuandikia kwakuwa uliopo hautoshelezi.
Kwa mujibu wa mkuu wa shule hiyo Enock Abraham amesema madarasa hayo yanatarajiwa kukamilika Februari 15 mwaka huu na kupelekea mkuu huyo wa mkoa kuahidi kufika shuleni hapo Februari 18 ili kukamilisha zoezi hilo.
Pia amewataka wanafunzi wa shule hiyo pamoja na walimu kutunza rasilimali zilizopo shuleni hapo ili zije kusaidia vizazi vijavyo kwani rasilimali hizo zinagharimu fedha nyingi hivyo ni vyema kukawa na umakini wa kuzilinda.
Ameongeza kuwa hajaridhishwa na matokeo ya kidato cha nne shuleni hapo hivyo walimu wajitahidi kuwafundisha wanafunzi kwa njia tofauti ikiwemo kuwasaidia wale ambao wanaelewa taratibu ili kuweza kukuza kiwango cha ufauru.
” Kuna wanafunzi wana uelewa wa tofauti ambapo mwingine ukifundisha tu ameshadaka na kuweka kichwani lakini mwingine ni mgumu kuelewa kwa haraka ambaye anatakiwa kufundishwa kwa utaratibu ndipo aelewe hivyo walimu mnapaswa kuwasaidia hao pia ili nao waweze kufanya vizuri”, Alisema Rubirya.
Katika msafara huo wa Dk. Awasi aliambatana na viongozi mbalimbali wa CCM ngazi ya mkoa pamoja na wilaya, wajumbe wa kamati ya siasa mkoa na wilaya pamoja na wakuu wa idara mbalimbali za serikali wa wilaya ya Ludewa.