Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala akizungumzia kuhusiana na maombi hayo leo Februari 6, 2021 makao makuu ya huduma hiyo yaliyop Yespa, Kihonda mjini Morogoro.
KIONGOZI Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala ametangaza Operesheni Ombeni Bila Kukoma ambayo imedhamiria kutoa dozi ya tiba kwa magonjwa yote yanayowatatiza Watanzania yakiwemo ya upumuaji katika mfumo wa hewa.
Ameyasema hayo leo Februari 6, 2021 makao makuu ya Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yaliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro wakati akizungumzia juu ya operesheni hiyo ambayo itafanyika mfululizo ili kumweleza Mungu hitaji la Watanzania kwa sasa.
Nabii Joshua amesema, operesheni hiyo inaenda sambamba na ile ya Ombea Taifa (Pray for Nation) ambayo aliiasisi miaka kadhaa iliyopita na imeleta mafanikio makubwa katika Taifa ikiwemo kuwaponya maelfu ya Watanzania.
“Tunakwenda kuongozwa na neno la Mungu kutoka 1 Wathesalonike 5:17, Biblia inaeleza kuwa, “ombeni bila kukoma”. Nasi tunakwenda kuomba bila kukoma ili Mungu wetu ambaye ndiye muumba Mbingu na nchi aweze kutuondolea changamoto zote za kiafya na mambo mengine yanayotukabili kwa sasa na hakika Mungu anakwenda kujibu maombi yetu,”amesema Nabii Joshua.
Amesema, operesheni hiyo Februari 13 hadi 14, 2021 itawakutanisha maelfu ya Watanzania katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo Chuo cha Mipango jijini Dodoma.
“Tunakwenda kutumia siku mbili katika makao makuu ya nchi, ili tumweleze Mungu kuwa,hitaji letu kuu kwa sasa ni kuliondolea Taifa letu magonjwa ya upumuaji katika mfumo wa hewa, kuuponya uchumi wetu na kuendelea kuwapa maono chanya viongozi wetu chini ya Rais Dkt.John Magufuli ili waendelee kutuongoza kwa hekima na maarifa.
“Hatua ambayo tangu awali imetuwezesha kupiga hatua kubwa kiuchumi na kila mmoja anashuhudia mabadiliko makubwa kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati na mingine mingi, Tanzania kwetu Mungu ndiye kimbilio letu, hatuna tegemeo zaidi yake kwa kuwa yeye ndiye mlinzi, mponyaji na mtoaji wa baraka kwa Taifa na hata jamii,”amefafanua Nabii Joshua.
Katika hatua nyingine, Nabii Joshua amesema kuwa, huu ni wakati wa kujinyenyekeza mbele za Mungu kwa kuwa, kila amtegemeaye Mungu huyashinda mambo yote.
“Mbali na hayo, leo tarehe 6 na 7, Februari,mwaka huu, hasira ya Bwana itawaka juu ya watesi wako, hivyo kwa pamoja tufike hapa Sauti ya Uponyaji Tanzania, Mungu akatutendee mema,”amesema.
Amesema, maelfu ya Watanzania wanatarajiwa kukusanyika katika Huduma ya Sauti ya Uponyaji iliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro kwa ajili ya kuliombea Taifa na viongozi wake.
Ibada hiyo itaenda sambamba na maombi kwa viongozi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na Rais Dkt.John Magufuli akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Wakati huo huo, Nabii Joshua amewaomba wakuu wetu wa nchi kuendelea kumtegemea Mungu kwa kila jambo wanalotaka kulifanya katika Taifa letu kwa kuwa, moyo huo unaenda kuwashangaza maadui wengi ambao wanainenea mabaya Tanzania.
Amesema, anaendelea na mfululizo wa maombi ya kuwakabidhi viongozi hao, wasaidizi wao na Watanzania mbele za Mungu ili Mungu aweze kuwashindia changamoto na majaribu mbalimbali ambayo wanapitia.
“Katika kitabu cha Yeremia 33:3, Biblia inasema, niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.
“Maneno haya ni Mungu aliyazungumza kwa kinywa cha Yeremia, alipokuwa katika gereza alilokuwa amefungwa, wakati huo Mji wa Yerusalemu ulikuwa umeshazungukwa na majeshi ya Nebukadneza na ndani ya mji kuna njaa kali.
“Lakini kama Biblia inavyosema katika kitabu cha Maombolezo 3:31,Mungu hatamtupa mtu hata milele. Maana yake ni kwamba kutakapotokea mitikisiko hata mtu akageuka na kumwacha Mungu na mtu yule akaadhibiwa katika dhambi zake, na mtu yule akatubu mbele za Mungu.