Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Dk Leonard Akwilapo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia (MAKISATU) ambayo yanatarajiwa kufanyika mwezi machi mwaka huu.
Mkuerugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dk Amos Nungu,akieleza kuhusu Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia (MAKISATU) ambayo yanatarajiwa kufanyika mwezi machi mwaka huu.
Mkurugenzi Idara ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (WEST) Prof.Maulilio Kipanyula,akizungumzia kuhusu Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia (MAKISATU) ambayo yanatarajiwa kufanyika mwezi machi mwaka huu
…………………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imesema kuwa bunifu mbalimbali zinaweza kuibua uchumi endelevu kutokana na Teknolojia itakayozalishwa Nchini ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo Wabunifu.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 5,2021 Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusiana na mashindano ya Sayansi,Teknolojia na ubunifu(MAKISATU).
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza mwezi ujao kuanzia tarehe 20 hadi 26 kwa lengo la kutambua ,kuenzi na kuendeleza jitihada za wabunifu.
“Lengo la mashindano hayo ni kuweza kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu ili kuibua vipaji vya wabunifu na kuweza kutumika kutatua changamoto Katika jamii,”amesema Dk.Akwilapo
Hata hivyo Dkt.Akwilapo amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana 2019/2020 Wizara hiyo imeibua wabunifu wachanga 1066 ambapo Kati yao wabunifu 130 wameendelezwa na Serikali kutokana na vitu ambavyo wamevifanya ili bidhaa hizo ziweze kuwa biashara.
“Kati ya hizo bunifu 20 zimefanikiwa na kutumika kutatua changamoto za jamii huku 25 zikiwa Katika mchakato,”amesisitiza
Aidha amesema kuwa Wizara imeendelea kuhamasisha Wadau wa mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kuimarisha uratibu lengo kuendeleza bunifu hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi COSTECH Dkt.Amos Nungu amesema wamekuwa wakiendeleza wabunifu kwa kuwajengea uelewa ikiwa ni pamoja na kuwapa Mafunzo ili watoke katika ubunifu na kufanya kazi.
Mashindano hayo ya kitaifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu ni ya mara ya tatu kufanyika nchini hapa ambapo kwa Mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu ya MAKISATU mwaka 2021 ni ”Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Uchumi Endelevu”