Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko akiwasilisha mada kwa wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya Bungeni Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko akizungumza wakati wa semina na wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya walizowasilisha wakati wa kikao cha kamati hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akisisitiza kuhusu Ofisi hiyo kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo Bungeni Jijini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya Mhe. Dkt. Alice Karungi Kaijage akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa Semina kwa wajumbe hao iliyoandaliwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).
Sehemu ya wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya wakifuatilia uwasilishwaji wa mada kuhusu masuala ya UKIMWI iliyolenga kuwajengea uwezo iliyandaliwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI yaliyofanyika Bungeni Jijini Dodoma.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya Mhe. Justine Nyamoga akiuliza swali wakati wa kikao cha kamati hiyo.
…………………………………………………………………………………………
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Tume ya Taifa ya kudhibiti Ukimwi hapa nchini TACAIDS imesema hali ya mapambano dhidi ya maambukizi ya virus vya ukimwi VVU hapa nchini imeendelea kuimarika, huku ikionyesha katika maambukizi mapya mengi yanayogundulika ni kundi la vijana wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 24.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya taifa ya kudhibiti maambukizi ya virus vya Ukimwi Dkt Leonard Maboko wakati akiwasilisha ripoti ya hali ya maambukizi ya ukimwi kitaifa na kimataifa kwenye Kamati ya kudumu ya Bunge ya maswala Ukimwi na dawa za kulevya.
Amesema hali ya maambukizi mapya ya virus vya ukimwi hapa nchini imepungua kwa kiasi kikubwa kwa mwaka 2019 watu wazima kuanzia miaka 15 ni takribani 68,484 kati yao wanawake 39, 614, wanaume 28,870 na Watoto chini ya miaka 15 ni 8600 jumla yake ikiwa ni 77, 084.
Licha ya takwimu kupungua lakini ripoti imeonyesha katika maambukizi mapya yanayoripotiwa ni kundi la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 ambapo maambukizi yamefikia asilimia 40 na kati ya hao kundi linaloathirika zaidi ni kundi la vijana wa kike ambapo ni asilimia 80.
“licha ya kuonyesha kuwa maambukizi yameshuka kwa kiasi kikubwa lakini maambukizi mapya yanakimbilia kwa vijana na hasa vijana wa kike, kati ya vijana 10 wenye VVU 8 ni wakike” amesema Maboko.
Aidha amebainisha kuwa hali ya maambukizi kwa hapa nchini hadi mwaka 2019 ilikadiriwa kuwa watu wazima 1,612,301 kati yao wanawake 983,471, wanaume 628,830 na Watoto chini ya miaka 15 ilikuwa 93,000, jumla ilikadiriwa kuwa 1,705,301.
Pia amesema vifo vitokanavyo na ukimwi kwa mwaka 2019 watu wazima ilikuwa 21,529, wanawake 9,304 , wanaume 12, 225 na Watoto chini ya miaka 15 kuwa ni 5,900, na jumla yake ni 27,429 akifafanua kuwa kundi la wanaume kupata vifo vingi kwa sababu ya kutokuzingatia dawa za kufubaza VVU.
Ameongeza kuwa “Trendi ya watu wanaoishi na virus vya ukimwi inaweza kuongezeka sana kutokana na watu kujitokeza kwa wingi kupima na kufuata ushauri wa wataalumu namna ya kuishi na virus vya ukimwi na hii ni kutokana na vifo vitokanavyo na ukimwi kupungua kwa kiasi kikubwa” amesema.
Aidha ameongeza kuwa kwa sasa kumekuwa na muamuko mkubwa sana wa watu kupima na kupokea majibu yao na kukubaliana na hali waliyonayo tofauti na miaka ya nyuma ambapo ilikuwa vigumu mtu kupima na kupokea majibu.
Maboko ameongeza kuwa “kampeni na huduma za kupima maambukizi ya VVU zimeendelea kuboreka, kwa mwaka 2019 zaidi ya watu milioni 10 walipata huduma za kupima VVU na kati yao 237,708 walibainika kuwa na VVU.
Amesema takwimu kidunia tangu janga la ukimwi kugundulika takribani watu milioni 75.6 wameambukizwa virus vya Ukimwi huku watu milioni 32.7 tayari wamekufa kwa maradhi hayo, aidha hadi kufikia Disemba 2019 watu milioni 38 walikuwa wanaishi na virus vya Ukimwi.
Awali akimuwakilisha Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, kazi, ajira, Vijana na watu wenye ulemavu Mhe Jenista Mhagama, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughurikia watu wenye ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amesema pamoja na kupungua kwa maambukizi ya VVU lakini takwimu zinasema watu takribani elfu 87 na 84 huambikizwa VVU kila mwaka.
Amesema ili kuimarisha udhibiti wa maambukizi ya VVU Serikali iliunda tume ya kudhibiti Ukimwi TACAIDS ili iweze kuratibu na kutekeleza hafua za ukimwi hapa nchini, tangu kuanzishwa kwa TACAIDS imeweza kujenga mahusiano kitaifa, kimataifa na kikanda ili kukabiliana na maambukizi ya VVU.
Amesema tangu kuanzishwa kwake imeweza kufanya tathmini na ufuatiliaji na kutoa elimu kuhusu sharia ya ukimwi na kutoa elimu kwa jamii kutambua afya zao na ushauri wa namna ya kuishi na virus vya ukimwi kwa walioambukizwa tayari, na namna ya kujikinga kwa ambao hawajaambukizwa kirusi vya ukimwi.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya maswala ya Ukimwi na dawa za kulevya wameitaka Serikali kuweka mkazo katika kutoa elimu hasa kwa vijana ili kuepusha idadi kubwa ya maambukizi ambapo takwimu zinaonyesha kundi la vijana ndilo linaloathirika kwa kiasi kikubwa kwa sasa.