MWAKILISHI wa Viti Maalum Mkoa wa Magharib Mhe. Fatma Ramadhan Mandoba, akimkabidhi zawadi mbalimbali Katibu wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar Ndg. Waziri Mbwana kwa ajili ya sherehe ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi kinachotimiza miaka 44.
MWENYEKITI wa Baraza la Wazee CCM Zanzibar Ndg. Khadija Jabir, akizungumza na Wajumbe wa Baraza hilo wakati akimkaribisha Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Magharib Mhe. Fatma Ramadhani Mandoba aliyewatembelea Ofisini kwao Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.
********************************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MWAKILISHI wa Viti Maalum Mkoa wa Magharibi Unguja,Fatma Ramadhani Mandoba, amewaomba Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kuwaelekeza,kuwashauri na kutoa nasaha kwa Wana CCM ili kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya Chama.
Ombi hilo amelitoa leo (jana) katika ziara yake ya kutembelea Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar lililopo katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, amesema mafanikio yaliyofikiwa nchini yametokana na juhudi kubwa za kiutendaji zilizoasisiwa na wazee hao ambao ni viongozi,watumishi na makada wa zamani.
Mhe.Fatma, alisema pamoja na majukumu waliokuwa nayo wazee hao bado wanatakiwa kuendelea kutoa nasaha na miongozo yao juu ya masuala mbalimbali ya kiuongozi na kiutendaji kwa nia ya kuimarisha Chama na Jumuiya zake.
Alieleza kwamba lengo la ziara hiyo ni kujumuika na Wazee hao kusherehekea miaka 44 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi ambapo, kwa kipindi hicho chote chama kimepitia vipindi mbalimbali vya mafanikio na maendeleo endelevu.
“ Wazee wangu nimekuja kwenu kwanza kupata Baraka zenu, pia kujumuika nanyi kutathimini na kusherehekea miaka 44 ya kuzaliwa kwa Chama chetu ambacho kimeleta heshima na kulinda haki na utu wetu kupitia Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.”, aliseleza Mwakilishi huyo Fatma.
Pamoja na hayo aliwakumbusha Wazee kwamba kwa sasa nchi inakabiliwa na vitendo vya mmomonyoko wa maadili hasa kuongezeka kwa vitendo vya ushalilishaji wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto , hivyo wazee hao nao wanayo nafasi ya kukemea na kutoa nasaha juu ya tabia hizo za kihalifu.
Alifafanua kuwa Wazee wanaweza kutoa mifano na historia za utamaduni wa wananchi wa visiwa vya Zanzibar namna walivyoishi kwa upendo,malezi na maadili mema ili vizazi vya sasa wajifunze na kuachana na maadili yasiyofaa.
Aliahidi kwamba kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ataendelea kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kutetea kikamilifu haki na maslahi ya wanawake na watoto katika chombo cha kufanya maamuzi.
Kupitia kikao hicho alimshukru Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, kwa ahadi yake ya kuimarisha maslahi ya Chama pamoja na pencheni za Wazee.
Pamoja na hayo alitoa zawadi ya vyakula mbalimbali kwa wazee hao ili washerehekee vizuri sikukuu ya kuzaliwa kwa CCM, ambayo kilele chake kinatarajiwa kufika kesho February 5, mwaka 2021.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Khadija Jabir, amesema kuwa ushauri uliotolewa na kiongozi huyo kutoka jumuiya ya Wazazi wataufanyia kazi ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya Chama na Serikali zote mbili.
Alisema Wazee hao wamekuwa wakitoa nasaha mbalimbali kwa Wana CCM juu ya masuala mbalimbali ya kuimarisha Chama sambamba na kutoa matamko juu ya vitendo vinavyoashiria uchochezi na uvunjifu wa Amani.
“Tunashukuru sana kwa ujio wako kwani tumeweza kupata faraja juu ya nasaha zako kwani Baraza hili lipo kwa ajili ya wanachama wote, hivyo mkitukumbuka kwa kuja kuchota maarifa na busara zetu tunajiona bado mnatuthamini sana”, alisema Bi. Khadija.
Ziara hiyo inatokana na sherehe za wiki ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi kilichoasisiwa February mwaka 1977, baada ya kuungana kwa vyama viwili vya ukombozi ambavyo ni TANU na ASP.