Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Waitara akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo Januari 4, 2021 wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika Kikao cha tatu Mkutano wa 2 wa Bunge la 12.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu (kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wake Mhe. Mwita Waitara 2021 wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika Kikao cha tatu Mkutano wa 2 wa Bunge la 12.
**********************************************
Tanzania imepokea kiasi cha Dola za Marekani10,008,564kutoka katika Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund – AF) chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa ajili ya kutekeleza miradi mitano.
Hayo yalisemwa jana bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Waitara wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Donge Mhe. Soud Mohamed Jumah aliyetaka kufahamu kiasi cha fedha Tanzania ilichoomba na kupewa kutoka Mfuko huo.
Waitara aliitaja miradi iliyonufaika na fedha hizo kuwa Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Mkoa wa Dar es Salaam wenye kwa gharama ya Dola za Marekani 5,008,564 ambao ulitekelezwa mwaka 2013 hadi 2019 kupitia fedha zilizotolewa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP).
Alibainisha kuwa kazi zilizofanyika katika mradi huo ni ujenzi wa ukuta wa kukinga maji ya bahari maeneo ya Kigamboni na Barabara ya Barack Obama, pamoja na ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua katika manispaa za Ilala na Temeke na kupanda mikoko Mbweni na Kigamboni.
Pia Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa jamii za pwani ya Zanzibar wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1zimeidhinishwa na Bodi ya Adaptation Fund (AF) na kiasi cha Dola za Marekani 30,000 kilitolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi.
Aliongeza kuwa fedha zitatolewa kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambayo ziiliwasilisha kwa mtekelezaji wa mradi huo ambaye ni Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar na kuwa taratibu za kusaini mkataba kati ya NEMC na Mfuko wa AF zinaendelea chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Akiendelea kujibu swali hilo alisema Mradi wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa Jamii za Wakulima na Wafugaji Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 1.2 ambao tayari umeidhinishwa na Bodi ya AF na kiasi cha Dola za Marekani 30,000 kimetolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi Fedha zitatolewa kupitia NEMC na kuwasilishwa kwa mtekelezaji ambaye ni Asasi ya Foundation for Energy Climate and Environment (FECE) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
“Mradi wa Kimkakati wa Teknolojia ya Kuvuna Maji Kuimarisha Uwezo wa Jamii za Vijijini katika Maeneo Kame ya Mikoa ya Singida, Tabora na Dodoma kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 1.2 ambao pia umeidhinishwa na Bodi ya AF na kiasi cha Dola za Marekani 30,000 kimetolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi. Fedha zitatolewa kupitia NEMC na kuwasilishwa kwa mtekelezaji ambaye ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Halimashauri husika za Bahi, Manyoni na Nzega,” alisema.
Aidha Waitara alitaja mwingine ulionufaika ni Mradi wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Wilayani Bunda mkoani Mara kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 1.4 ambapo mradi huu bado haujaidhinishwa na Bodi ya AF lakini kiasi cha Dola za Marekani 30,000 kilitolewa kwa ajili ya kuandika andiko la mradi huku fedha hizo zilkipokelewa kupitia NEMC na kuwasilishwa kwa Halmashauri hiyo na kuwa Bodi ya AF itapitia mradi huo na kuufanyia maamuzi katika kikao chake cha Machi 2021.