***********************************
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Kibaha Mji ,mkoani Pwani ,limepitisha bajeti ya mapato ya matumizi kwa mwaka 2021-2022 kiasi cha sh.bilioni 36.220 ,katika vyanzo mbalimbali vya mapato .
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ,Selina Wilson alisema ,kiasi hicho mapato ya ndani ni sh .bilioni 3.937 na ruzuku toka Serikalini ni sh.bilioni 31.734.724 .
Kati ya bajeti hiyo iliyopitishwa pia ,sh.bilioni 22.237 ni mishahara na bilioni 1.299.312 ni matumizi ya kawaida ambapo miradi ya maendeleo itatumia sh.bilioni 8.198.390.263.
Akizungumza katika baraza hilo ,diwani wa kata ya Kongowe Hashim Shomari alisema wameanza ujenzi wa kituo cha afya,eneo la Miembe Saba shule , kwa nguvu za wananchi ili kuondoa kero ya kufuata huduma mbali hospital ya Tumbi,hospital ya wilaya ya Lulanzi ama Mkoani ambako wanafuata huduma hiyo sasa .
Shomari aliiomba ,halmashauri iangalie namna ya kuunga mkono juhudi hizo baada ya wananchi kuonyesha nia.
Kwa upande wake ,diwani wa viti maalum Lydia Mgaya alitaka wadau mbalimbali washirikishwe katika kuchangia sekta ya elimu ili kupunguza changamoto zilizopo.
Diwani wa kata ya Pichandege Karim Mtambo ,alieleza itakuwa vyema endapo kitaboreshwa stendi kuu ya mabasi kwa kuweka vivutio ,taa za kutosha na kuwaondoa wasioendeleza viwanja eneo linalozunguka stendi hiyo .
Doris Michael ambae ni diwani viti maalum aliomba ,elimu itolewa kuhusiana na mabadiliko ya utaratibu mpya wa mikopo kwa vifaa badala ya fedha kwa baadhi ya miradi.