Home Mchanganyiko CHIKOTA AITAKA SERIKALI KUWEKA MKAKATI WA PEMBEJEO ZA ZAO LA KOROSHO KUPATIKANA...

CHIKOTA AITAKA SERIKALI KUWEKA MKAKATI WA PEMBEJEO ZA ZAO LA KOROSHO KUPATIKANA KWA WAKATI

0

……………………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

Mbunge wa Nanyamba kupitia chama cha Mapinduzi CCM Mhe. Abdallah Chikota ameishauri Serikali kuweka mkakati kabambe wa kuhakikisha pembejeo zinazotumika katika zao la korosho kuwafikia wakulima kwa wakati na kwa bei nafuu.

Mhe Chikota ametoa ushauri huo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa bungeni wakati akifungua rasmi Bunge la 12, ambapo Mhe. Chikota amesema Rais Dkt Magufuli katika hotuba yake alisisitiza kilimo chenye tija na kuahidi upatikanaji wa pembejeo na viatilifu kwa wakati.
“Sisi Mtwara zao kuu la uchumi ni korosho, naomba serikali kuwa na mkakati maalum wa kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu, Tuhakikishe zao la korosho tunapanua soko lake, kuna minada inayoendelea lakini kuna TMX sasa hivi wanashiriki wanunuzi wale wale wanaoingia minadani hebu TMX iwezeshe ili tuwapate wanunuzi wakubwa kutoka Vietnam na China,” amesema.
Aidha ameiomba Serikali kujielekeza katika kuwawezesha wabanguaji wadogo ili waongeze thamani kwenye korosho zao badala ya kuuza korosho ghafi hali inayosababisha kuuza kwa bei ndogo.
Akizungumzia suala la miondombinu, Mhe. Abdallah Chikota ameomba serikali kutafuta chanzo kingine cha fedha ili kuiongezea fedha Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini(TARURA) ili ifanye kazi yake kwa ufanisi zaidi.
“Barabara yetu ya ulinzi, niipongeze kamati yetu ya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi nzuri kwenye mpaka wa Tunduma sasa naomba barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami, kutoka Mtwara hadi Mbinga, ni barabara muhimu kwa ulinzi na usalama wa nchi,” amesema.
Akizungumzia kiwango cha tozo za meli amesema katika bandari ya Mtwara amesema “Ukiifanya bandari ya Dar es salaam na Mtwara kuwa na rate sawa hii haitawavutia kupeleka meli Mtwara, naomba kuwe na kiwango maalum ili kuwavutia wawekezaji kuleta meli Mtwara,” amesema.
 Kuhusu suala la maji katika jimbo la Nanyamba Mhe. Chikota, ameiomba serikali kutumia maji ya mto Ruvuma kujenga miradi mikubwa ya maji ili maji yawafikie wananchi wengi.