************************************************
Na Mwandishi wetu, Kiteto
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU, imemfikisha Mahakamani mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Orkitikiti, Kijiji cha Engong’ongare Wilayani Kiteto, Oscar Waluye na kusomewa mashtaka ya udanganyifu wa mtihani.
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Alli Sadiki Hajji akizungumza na waandishi wa habari amesema pia, mwalimu huyo Waluye, amefukuzwa kazi na mamlaka yake ya nidhamu.
Hajji amesema Waluye ameshtakiwa kwa kufanya udanganyifu katika mtihani wa darasa la saba iliyofanyika Oktoba 2020 kitendo ambacho ni kinyume cha kifungu cha 23 na 24 (1) sheria ya baraza la mitihani la Taifa.
Amesema kesi hiyo ya jinai imefikishwa mbele ya hakimu mfawidhi wa wa mahakama ya wilaya ya Kiteto, Joakim Mwakyolo na mwendesha mashtaka wa polisi Wilfred John.
“Hata hivyo, amekana shtaka hilo na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo kupelekwa rumande na kesi hiyo itatajwa tena Februari 16 mwaka huu,” amesema Hajji.
Amesema uchunguzi wa TAKUKURU Wilayani Kiteto umeonyesha kwamba Waluye aliwalazimisha wanafunzi wawili wa darasa la sita wa shule hiyo kufanya mitihani ya darasa la saba badala ya watahiniwa ambao uwezo wao darasani unaelezwa ni wa kiwango cha chini.
“Pia Waluye alimkaririsha mwanafunzi mmoja aliyehitimu shuleni japo mwaka 2019,” amesema Hajji.
Amesema wanafunzi hao wawili wa darasa la sita na mmoja wa darasa la saba aliyehitimu mwaka 2019 walikamatwa na makachero wa TAKUKURU tayari wakiwa wamefanya mitihani ya masomo ya Kiswahili na Hisabati kwa niaba ya wanafunzi wenzao wanaodaiwa kuwa na uwezo mdogo huku aliyekaririshwa akifanya mtihani wa mwanafunzi mtoto.
Amesema katika mahojiano na maofisa wa TAKUKURU Wilayani Kiteto, Waluye alikiri kutenda makosa hayo kwa maelezo kuwa alitaka shule hiyo ionekane imefaulisha vizuri.
“Kitendo hicho ni kinyume cha maadili kwa kuwa kinawajengea watoto ambao ni Taifa la kesho tabia za ukiukwaji wa maadili na wakati wote kuwa tegemezi,” amesema Hajji.
Ametoa rai kwa wazazi, walezi na walimu kuwalea watoto katika njia iwapasao kwani hawataiacha hata watakapokuwa wazee (Biblia Mithali 22:6).
“Nitumie nafasi hii kuwafahamisha watumishi wa umma Mkoani Manyara kwamba kuanzia sasa watakaodhihirika kutenda makosa ya jinai na Rushwa tutakuwa tunawafikisha kwanza kwenye mamlaka zao za nidhamu na kuwashtaki kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma na wasiendelee kupokea mishahara bila kuifanyia kazi,” amesema Hajji.
Amesema baada ya kuondolewa kwenye utumishi, mashtaka ya jinai yatafuata kama ilivyofanyika kwa Mwalimu Waluye kwa kuwa jinai haina ukomo.