*********************************************
Kocha msaidi wa Timu ya KMC FC , Habibu Kondo amesema kuwa anakiamini kikosi chake katika kuelekea kwenye mchezo wa Kiporo dhidi ya Namungo utakaopigwa kesho saa 10.00 jioni katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Kondo amesema kuwa kikosi hicho cha wana Kino Boys kimeshafanya maandalizi ya kutosha kuelekea katika mtanange huo na kwama hana hofu kwani viongozi na benchi zima la ufundi limejipanga vyema kuhakikisha kwamba alama tatu zinabaki katika Timu ya KMC FC.
Katika mchezo huo ambao KMC ni wenyeji, Kocha Habibu amesema kuwa licha ya kwamba Namungo ni timu nzuri lakini KMC FC ni nzuri na bora zaidi yao na hivyo kila mmoja atapata matokeo kulingana na maandalizi.
Ameongeza kuwa kwasasa kikosi cha KMC kimeimarika zaidi ikiwa ni baada ya kuongeza wachezaji wawili katika usajili wa Dirisha dogo na kwamba ladha ya mpira kutoka kwa vijana wa Kinondoni inarudi katika safasi yake na kwamba mashabiki na wapenzi wa KMC wajiandae kupata ushindi katika michezo yote ya Ligi kuu Soka Tanzania bara.
“ Ni muda sasa hatujacheza mechi, ukiacha zile za kirafiki ambazo tulikuwa tunacheza, lakini bado Timu yetu ipo kwenye ubora wake, na kesho tunaingia uwanjani tukiwa na uhakika wa kupata matokeo mazuri, tunajua Namungo ni Timu nzuri lakini sisi ni wazuri zaidi yao” amesema Kocha Habibu.
Hadi sasa KMC FC ipo katika nafasi ya saba ikiwa imecheza michezo 17 na kwamba mkakati ni kuhakikisha kuwa mechi Timu inashinda mechi zote zilizosalia katika duru ya pili ya lala salama.