**************************************************
Na Damian Kunambi, Njombe
Kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wazazi wa wanafunzi wa shule za sekondari wilayani Ludewa mkoani Njombe juu ya kiwango cha uchangiaji chakula kwa wanafunzi hao, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratias amesema kuna haja ya kuweka kiwango maalum ambacho kitatumiwa kwa shule zote wilayani humo.
Hayo ameyasema alipotembelea wakuu idara ya elimu akiwa sambamba na kamati ya siasa ya Chama cha mapinduzi (CCM) wilayani humo ambayo ilifanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ikiwa ni wiki ya maadhimisho ya sherehe ya kutimiza miaka 44 kwa chama hicho.
Akijibu hoja ya mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo Stanley Kolimba baada ya kueleza kwa jinsi gani wazazi wanavyotoa michango mingi ya chakula ambapo kila shule imeweka kiwango chake cha uchangiaji ambapo shule nyingine zimekuwa zikipokea debe 12 hadi 14 za mahindi kwa mwanafunzi mmoja kwa mwaka.
Kolimba aliongeza kuwa kutokana na wingi huo wa chakula kinachopelekwa katika shule hizo husababisha wazazi kuwa na hisia tofauti kuwa huenda mahindi mengine hurudishwa mtaani kwaajili ya kuuzwa kwakuwa kwa mwanafunzi mmoja si rahisi kumaliza debe 12 kwa mwaka mmoja ukizingatia kuna likizo pia.
Mkurugenzi amesema atakaa na wakuu waidara ya elimu msingi pamoja na sekondari ili kuona tatito liko wapi kisha watatoa muongozo wa uchangiaji chakula ambao utatakiwa kufuatwa kwa shule zote za wilaya hiyo.
Aidha kwa upande wa katibu wa chama hicho wilayani humo Bakari mfaume aliwashauri wakuu wa idara hiyo pamoja na mkurugenzi kufuatilia kwa ukaribu walimu wanaohamishwa kwani kuna baadhi yao wanaenda kuripoti maeneo waliyohamishiwa kisha wanarudi kusubiri stahiki zao.
Amesema stahiki zinapochelewa hupelekea kuonekana kuna upungufu wa walimu kumbe kuna wengine wapo mtaani kwa muda wa mwaka mzima na zaidi hawafanyi kazi huku mshahara wanapokea kwa madai kuwa wanasubiri stahiki zao ndipo wakaanze kufanya kazi katika vituo walivyohamishiwa.
“Nikweli Ludewa ina changamoto ya uchache wa walimu lakini upungufu mwingine husababishwa na walimu wanaohamishwa kutoripoti kwenye vituo huku mishahara wanachukua, nawaomba sana wakuu wa idara hii mhakikishe mambo haya hayajitokezi na muwaambie walimu wenu kuwa wanapohamishwa waende kufanya kazi stahiki zao zitawakuta huko huko”, alisema Mfaume.