*******************************
Feb 3
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini,mkoani Pwani, kimejiwekea mkakati wa kuongeza wanachama zaidi kwa mwaka 2021-2022 ,ikiwa ni pamoja na kumtaka kila balozi kuongeza wanachama wapya 25.
Aidha ,kimehimiza umoja na mshikamano kwa wanachama wake ili kukiimarisha chama hicho .
Akizungumzia sherehe za kuadhimisha miaka 44 ya CCM tangu kuanzishwa kwake ,Katibu wa CCM Kibaha Mjini ,Afidu Luambano alisema mji huo una jumla ya mabalozi 611 hivyo kwa kila mmoja kupata wanachama wasiopungua 25 watakuwa wamepiga hatua kubwa.
Alibainisha, mabalozi ndio nguvu ya chama ,hivyo wataendelea kushirikiana nao kwa kuhakikisha mikakati ya chama inafanikiwa na chama kinasonga mbele.
“Chama chochote mtaji wake ni kuongeza wanachama wapya ambapo mwaka 2018 walikuwa na wanachama 39,000 na hadi kufikia 2019 Katika uchaguzi wa serikali za mtaa,vijiji na vitongoji waliongezeka na kufikia 53,230.” alifafanua Luambano.
Luambano aliwaasa wanachama na viongozi wa kata pia kuwa na ushawishi kuongeza wanachama na kusisitiza umuhimu wa kulipa ada .
Pamoja na hayo alikemea makundi yasiyo na tija na kuomba umoja na mshikamo uzidishwe baina yao .
Akielezea ,sherehe za kuadhimisha miaka 44 ya CCM ,Katibu huyo alisema, wanahimiza kila kata kuchangia madawati mawili kwa ajili ya kuchangia kupunguza tatizo la upungufu wa madawati kwenye shule za sekondari ama shule za msingi Mjini hapo .
Hata hivyo ,kata itakayofanikiwa kwa maandalizi mazuri ya sherehe za maadhimisho ya miaka 44 ya chama kitatoa zawadi ikiwa ni kama motisha .