Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashauri wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Jerry Mwaga akijibu hoja mbalimbali za Madiwani jana .
…………………………………………………………………………………………………….
NA TIGANYA VINCENT
UONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua imepiga marufuku kwa Watendaji wa Vijiji kuwatoza shilingi 1,000/= wafanyabiashara wa mifugo wanapokuwa wanapeleka minadani.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashauri hiyo Jerry Mwaga wakati Baraza la Madiwani alipokuwa akijibu hoja ya Madiwani waliolalamika Watendaji wa Vijiji kuwatoza wanyabiashara wa mifugo gharama za usafirishaji wa ng’ombe kabla hajauza ng’ombe wao.
Alisema mfugaji haruhusiwi kutozwa kiasi chochote cha fedha kipindi anaposafisha mifugo kwenda mnadani kwa ajili ya kuuza ng’ombe na pale anapokuwa anarudisha ng’ombe ambazo hazikununuliwa.
Mwaga alisema mifugo inatakiwa kutozwa kwenye eneo la Mnada husika na sio vinginevyo na kuwataka Watendaji wa Kata kusimamia utekelezaji wa agizo hilo ili wafugaji wasitozwe fedha kinyume cha utaratibu.
Aliwaomba Madiwani kuangalia maeneo ambayo wanadhani yanafaa kwa uanzishaji Minada ili waweze kutuma Watalaamu wa Halmashauri kwenda na kufanya utafiti na pindi watakapobaini kuwa kuna tija waweze kutoa vibali.
Mwaga alisema suala la uanzishaji wa minada ni muhimu liibuliwe na wananchi wa eneo husika kwa ajili ya kuuwezesha kuwa endelevu na kuewezesha Halmashauri kuwa na chanzo cha uhakika cha mapato.
“Kama kuna wananchi wanataka kuwepo kwa mnada katika eneo lao wapeleke wazo katika Halmashauri ya Kijiji nayo itapeleka wazo hilo katika kikao cha Maendeleo ya Kata (WDC) ambacho nacho kitaandika kwa Halmashauri ya Wilaya na sisi tutawatuma wataalamu kwa ajili ya kuangalia eneo na kutoa kibali kwa ajili ya uanzishaji wa shughuli za minada” alisisitiza.
Alisema Minada ni muhimu katika uongezaji wa mapato ya Halmashauri lakini ni vizuri kama wazo litaanzia kwa wananchi katika eneo husika.