******************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Na MWANDISHI WETU
NAHODHA wa klabu ya Tanzania Prison inayoshiriki ligi Kuu Tanzania, Laurean Mpalile, ametangaza kutundika daruga ameamua kutangaza kustaafu soka baada ya kudumu kwa muda wa miaka minne kusakata kabumbu la kulipwa.
Akizungumza hivi karibuni na Mwandishi wetu Mpalile amesema ameamua kustaafu soka na kuwaachia vijana wapewe nafasi kwani yeye umri umeshaenda.
“Umefika muda muafaka wa mimi kupumzika nimecheza muda mrefu miaka 14 imetosha ngoja niwaachie vijana ili nao waoneshe uwezo wao”. Amesema Mpalile.
Amesema ataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau mbalimbali wa mpira wa miguu pamoja na uongozi wa klabu ya Tanzania Prison kwani ndio klabu iliyomfikisha alipo sasa katika maisha ya soka.
Pamoja na hayo Mpalile amesema kuna matukio mengi ambayo hatoacha kuyasahau katika maisha yake ya soka hasa tukio la kuipandisha klabu yake kushiriki ligi Kuu Tanzania bara baada ya kushuka mwaka 2010.
“Kiukweli matukio yapo mengi lakini kubwa nalolikumbuka ni siku ambayo tuliipandisha timu yetu ya Tanzania Prisons baada ya kushuka daraja”. Amesema Mpalile.