Diwani wa kata ya Luana Willbard Mwinuka ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati huduma za elimu idara ya elimu msingi akiwasilisha taarifa ya kikao cha kamati yake.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratius akiongea na baraza la madiwani katika kikao cha baraza hilo. Kulia kwake ni mwenyekiti wa halmashauri hiyo Wise Mgina, mkuu wa wilaya hiyo Andrea Tsere, makamo mwenyekiti wa baraza la madiwani Leodga Mpambalioto pamoja na mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ludewa.
Diwani wa kata ya Lubonde Edga Mtitu akihoji juu ya ulipaji stahiki za walimu wapya pamoja na kuomba walimu hao kuripoti katika vituo husika.
Madiwani wa kata mbalimbali za wilaya ya Ludwa wakifuatilia mijadala iliyokuwa ikiendelea katika kamati mbali za baraza hilo.
…………………………………………………………….
Na Damian Kunambi, Njombe.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilayani ya Ludewa iliyopo mkoani Njombe Sunday Deogratias amesema kutokana na mazingira magumu wanayofanyia kazi walimu wa shule mbalimbali wilayani humo wameweka mkakati wa kutoa motisha kwa walimu hao ikiwemo na kulipwa stahiki zao ili kuwapa nguvu ya kufundisha vyema.
Mkurugenzi huyo ameyasema hayo baada ya mwenyekiti wa kamati ya huduma za elimu idara ya elimu msingi Willbard Mwinuka kuwasilisha taarifa ya kikao cha idara hiyo katika kikao cha baraza la madiwani na kuulizwa swali na diwani wa kata ya Lubonde Edga Mtitu juu ya kuwapeleka walimu wapya katika vituo walivyopangiwa pamoja na ulipwaji wa stahiki zao .
Mkurugenzi huyo amesema kuwa kuna walimu wapya 48 walioletwa kwa shule za msingi na sekondari na tayari walishapangiwa vituo hivyo wanatakiwa kulipwa stahiki ya Sh. Ml. 16 kwa wote na tayari alikaa na afisa elimu msingi na sekondari pamoja na muweka hazina ili kujadili jinsi ya kuwalipa kwakuwa fedha hizo zinatakiwa kutoka serikali kuu.
Ameongeza kuwa kwakuwa kwa sasa serikali imejikita zaidi katika utekelezaji wa miradi mikubwa hivyo kama halmashauri wanapaswa kuona namna ambavyo watawalipa walimu hao na pindi fedha za serikali kuu zitakapoletwa watazirudisha mahali ilipotolewa.
” Kutokana na serikali kuu kuwekeza fedha nyingi katika miradi mbalimbali ambayo ni mikubwa hivyo ili tusiwape wakati mgumu walimu wetu wa kusubiri fedha hizo halmashauri tunatakiwa kutumia vyanzo vyetu kuwalipa na fedha za kutoka serikali kuu zitakapowasili basi tutazirudisha mahala zilipotolewa”, Alisema Deogratias.
Aidha amemshukuru rais John Pombe Magufuli kwa kuona upungufu wa walimu walionao na kuwaletea walimu hao 48 japo bado idadi hiyo haijakidhi uhitaji ila wanapaswa kumshukuru na wanaamini kwakuwa rais kaguswa na upungufu huo kutakuwa na uendelevu wa kuwaletea walimu wengine zaidi.
Naye mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye ni diwani wa kata ya Mundindi Wise Mgina alimtaka Mkurugenzi huyo kuhakikisha jambo hilo linatekelezwa kwa uharaka ili kutowafanya walimu hao kuwa wanyonge.
Aliongeza kuwa malipo hayo yanapochelewa hupelekea walimu kutokuwa na imani na serikali yao na kujihisi kuwa hawapewi kipaumbele na kutoonekana wamuhimu.
“Ili walimu hawa waweze kuwafundisha vyema watoto wetu na kwa moyo wa dhati wanapaswa kukamilishiwa stahiki zao kwa wakati ikiwemo kupewa motisha mbalimbali hii itawafanya kufundisha kwa bidii na kuyapenda mazingira yao ya kazi”, Alisema Mgina.