Na Dotto Mwaibale
WASANII wa Kikundi cha Sanaa cha Dofa kilichopo Karatu mkoani Arusha wanatarajia kumpokea Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa kwa wimbo maalumu katika kongamano la wanamuziki.
Bashungwa atakuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo la Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) litakalofanyika Februari 20, 2021 jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel alisema hivi sasa kikundi hicho kipo katika mazoezi ya wimbo huo maalumu kwa ajili ya kumpokea Waziri Bashungwa.
” Waziri Bashungwa anakuja kwenye kongamano letu wanamuziki hivyo tumeona ni lazima tumpokee kwa wimbo maalumu kwa ajili ya kumpa heshima.” alisema Joel.
Joel alisema katika kongamano hilo pamoja na mambo mengine Bashungwa atatoa kadi za Bima ya Afya ya NHIF kwa Wanamuziki wa kada zote na kusikiliza changamoto zao mbalimbali.
Alisema kadi hizo zitawasaidia kupata vipimo na matibabu katika hospitali za Serikali na binafsi.
“Serikali imetukumbuka wanamuziki kwa kutupatia kadi za bima ya afya ya Taifa kwa gharama nafuu kupitia Tanzania Music Foundation (TAMUFO) jambo litakalo tusaidia wanamuziki kupata matibabu.” alisema Joel.
Joel aliwataja baadhi ya wanamuziki watakao kabidhiwa kadi hizo kuwa ni wa muziki wa Injili, bongo fleva, dansi, taarabu na ngoma za asili.
Aidha Joel alisema kitendo cha Serikali kutoa kadi hizo za bima ya afya kwa wanamuzikini utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli ya kuwasaidia wasanii hapa nchini.
Katibu mkuu huyo wa TAMUFO alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kuelezea kuwa wamepata ari na nguvu mpya ya kutekeleza shughuli zao kwa vitendo kwa ajili ya maendeleo ya sanaa hapa nchini.
Alisema maandalizi yote ya kongamano hilo yamekwisha kamilika ikiwa na taratibu za kuwapata wanamuziki.
Joel aliongeza kuwa katika kongamano hilo maafisa kutoka Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na Maafisa Utamaduni na wadau wengine watakuwepo.