………………………………………………………………………
Na Damian Kunambi, Njombe.
Wanafunzi wilayani Ludewa mkoani Njombe wametakiwa kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika mitiani yao ya mwisho pasipo kusikiliza vishawishi vya wazazi vinavyowataka wafanye vibaya kwenye mitihani ili wakawasaidie shufguli zao mbalimbali.
Hayo ameyasema katibu wa mbunge wa jimbo la Ludewa Alphonce Mwapinga alipomuwakilisha mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga katika hafla ya kuwakaribisha kidato cha kwanza katika shule ya Nicopolis Academy na Andrea Tsere Open School iliyofanyika shuleni hapo.
Amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaambia watoto kuwa wasifanye vizuri katika mitihani yao ya mwisho kwa kukwepa majukumu yao ya kuwaendeleza kitu ambacho kinarudisha Maendeleo ya elimu wilayani humo.
“Ninawaasa msome kwa bidii ili muweze kufikia malengo yenu mnapaswa kuwasikiliza wazazi wenu kwa mambo mazuri watakayokuwa wanawashauri, lakini endapo watawashauri mfanye vibaya kwenye mitihani yenu ya mwisho ili kukwepa gharama ya kuwaendeleza kwa madai kuwa watawapeleka kusomea ufundi na wengine wakidai kuwa mkawasaidie shughuli za shamba, msikubali maana wanakatisha ndoto zenu”, Alisema Mwapinga.
Naye mkurugenzi wa shule ya Nicopolis Academy Augustino Mwinuka amesema kwa kushirikiana na Andrea Tsere open school wamekuwa wakipokea wanafunzi ambao waliishia njiani katika masomo yao na wanahitaji kujiendeleza ambapo walianza na wafunzi kumi na nne na sasa wanafunzi wamefikia 150 huku bado wakiendelea kupokea wanafunzi wengine.
Amesema kumekuwa na muitikio mkubwa kwa wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nje ya Ludewa hivyo amewataka wanaludewa kutumia fursa hii ya kuwapa elimu watoto wao kwakuwa shule binafsi zilizopo katika wilaya hiyo ni chache ukilinganisha na uhitaji wa wanafunzi.
Aliongeza kuwa shule yake imejipanga vyema katika kutoa elimu bora kwani imelenga kutoa msaada wa kuwapa elimu bure wanafunzi wasio jiweza na waishio katika mazingira magumu ambapo watoto hao watasoma bure bila kulipia gharama yoyote huku kwa wale wanaojiweza watalipia ada kidogo ili kuweza kuendesha shule hiyo.
“Shule hii tayari imejipanga kutoa elimu kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne pia kuna mkakati wa kuanzisha chuo cha ufundi hivyo tunaamini tutaweza kuwasaidia wanafunzi katika ngazi zote na kuwafanya waweze kutimiza malengo yao kielimu”, Alisema Mwinuka.
Aidha kwa upande wa mmoja wa wanafunzi hao Daniel Komba amesema wamekuwa wakifundishwa vyema na walimu wao japo wanakabiliwa na changamoto ya vifaa vya michezo hivyo wanaiomba serikali kupitia mbunge wao Joseph Kamonga kuwasaidia vifaa hivyo vikiwemo mipara na jezi.