Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
…………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Manyara
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka jana ilipokea jumla ya malalamiko 208, ambapo kati yao 127 yalihusiana na makosa ya rushwa na malalamiko 81 yalihusu makosa mengine.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya utendaji kazi wa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Makungu amesema kesi mpya zilizofikishwa mahakamani ni mbili, kati ya hizo moja inamuhusu Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Miomboni kupitia CCM, Mathias Zebedayo.
Amesema Zebedayo ameshtakiwa kwa kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 100,000 ili kusaidia kurejesha kiwanja kilichopo eneo la mtaa wa Miomboni wilayani Babati ambapo yeye ni Mwenyekiti wa mtaa.
Amesema ukiacha kesi hiyo, Zebedayo pia anatuhumiwa kutumia muhuri wa Mwenyekiti wa Miomboni kuuza ardhi mtaa wa Bagari Ziwani, kesi ambayo itafunguliwa mara baada ya uchunguzi utakapokamilika.
“Kesi zilizokamilika ni mbili ambapo washtakiwa wote walipatikana na hatia akiwemo mwandishi wa habari wa kujitegemea Patrick Chambo aliyehukumiwa kifungo cha miaka nane jela kutokana na kosa la kupokea rushwa ya shilingi 150,000 kinyume na kifungu cha 15 namba saba ya mwaka 2007,” amesema Makungu.
Amesema Chambo aliomba na kupokea rushwa hiyo kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Mati Super Brands ili asimuandike kwenye vyombo vya habari kutokana na tuhuma za kukwepa kodi alizokuwa nazo, mfungwa huyo Chambo ameanza kutumikia kifungo chake tangu Januari 21 mwaka huu baada ya kukamatwa Korogwe mkoani Tanga.
“Rai yetu wanahabari wanapokuwa na taarifa kama alizokuwa nazo Chambo wazitoe kwa mamlaka zinazohusika ili hatua zichukuliwe kwa faida ya jamii nzima badala ya kuzitumia kuomba rushwa kwa nia ya kujinufaisha wenyewe,” amesema Makungu.
Hata hivyo, amesema viongozi wa CCM wakubali kwa vitendo kuwa sehemu ya vita dhidi ya rushwa kama Jaji mkuu wa Tanzania, profesa Ibrahim Juma aliwahi kusema wakati akifungua kongamano la wadau wa kujadili mapambano dhidi ya rushwa katika mfumo wa utoaji haki Juni 17 mwaka jana.
Amesema Jaji Mkuu alisema kuwa utashi wa kisiasa na dhamira anayoonyesha Rais John Magufuli haitoshi bila ya kila taasisi, kila idara na kila mwananchi kukubali kwa vitendo kuwa sehemu ya vita dhidi ya rushwa.
“Ni rai yetu viongozi wa CCM Mkoani Manyara kukubali kwa vitendo kuwa sehemu ya vita dhidi ya rushwa kama ulivyo utashi wa kisiasa ulioonyeshwa na Rais Magufuli na wachukue hatua wasiwe ngao ya kuwakingia vifua,” amesema Makungu.