**********************************************
Anthony Ishengoma-Kahama
Rais John Pombe Magufuli ameitangaza Halmashauri ya Mji Kahama kuwa Manispaa wakati wa ziara yake Mkoani Shinyanga kujionea shughuli za Maendeleo mkoani humo na kuweka mawe ya Msingi katika Jengo la Utawala la Halmashauri ya mji huo na jengo la wagonjwa wa nje la Hospitali ya Mji kahama.
Huamzi huo pia ulichagizwa na hatua ya Halmashauri ya Kahama kutoa ardhi bure ili kuwavutia wawekezaji wa ndani jambo ambalo limemwemezesha mwekezaji wa ndani Bw. Muhoja Nkwabi kufungua kiwanda kikubwa cha vinywaji na usindikaji wa vyakula.
Rais Magufuli ameitaja Halmashauri ya Mji Kahama kuwa Halmashauri ya mfano hapa Nchini na kupongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Anderson Nsumba kwa kufanya kazi nzuri za kuendesha miradi mbalimbali kwa kutumia mapato ya ndani.
Pamoja na kuipandisha hadhi Halmashauri ya Mji Kahama kuwa Manispaa pia ametoa msamaha kwa Mkurugenzi Halmashauri hiyo kwa kosa la kununua gari la kifahari na kutaka arudishiwe gari hilo lakini asiendelee tena na tabia ya hiyo kutumia fedha nyingi katika manunuzi ya magari kama hayo.
Akiongea na wananchi wa Halmashauri ya Mji Kahama Rais magufuli amemwagiza Waziri wa Afya Bi. Doroth Gwajima kuipandisha hadhi ya Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kahama ili iendane na hadhi ya Hospitali za Manispaa.
Rais Magufuli pamoja na masuala mengine amewataka wananchi kote Nchini kuzalisha chakula kwa wingi ili hapo baadae waweze kujipatia mapato kutokana na nchi jilani ya Tanzania kujifungia kwa kuofia corona na hivyo kutoweza kuzalisha chakula cha kutosha hivyo kuwa fursa kwa watanzania kuuza mazao yao Nchi za nje.
Aidha Rais Magufuli amemwagiza Waziri wa viwanda na Biashara pamoja na Waziri mwenza wa Kilimo kuhakikisha wanaweka utaratibu utakaowawezesha wakulima mkoani Shinyanga kuuza mazao yao kwa faida baada ya Mbunge wa Kahama Jumanne Kishimba kudai Mkoa huo una ifadhi kubwa ya mchele imbayo imekosa wanunuzi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack katika salamu zake za Mkoa wa Shinyanga kwa Rais Magufuli ameomba Wizara ya Viwanda na Biashara kuruhusu Mkoa wa Shinyanga kubadili matumizi ya eneo la kiwanda cha nyama kugaiwa kwa wawekezaji kutokana na eneo hilo kukaa bila matumizi lakini pia kiwanda hicho kukosa wawekezaji kwa sasa.
Aidha Bi. Telack aliongeza kuwa Mkoa wake utaendelea kutoa mchango mkubwa kwa Rais Magufuli katika jitihada kubwa anazozifanya kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.
Rais Magufuli katika Ziara yake hiyo tayari ameweka jiwe la Msingi katika jengo la Utawala la Halmashauri ya Mji Kahama, Kiwanda cha Usindikaji wa Chakula cha KOM Group of Companies, Jengo la Wagonjwa wa Nje na anatarajia kufungua mradi wa maji Kagongwa Isaka.