*********************************************
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Idelphonce Mwambe (Mb), Leo tar 27 Januari, 2020 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) Ndugu, Leodegar Tenga.
Mhe. Mwambe mefurahishwa na jinsi taasisi za sekta binafsi zinavyoshirikiana na serikali ili kufikia adhma ya kuifanya nchi yetu kuwa ya Viwanda.
Aidha Mhe. Mwambe amesema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi hasa katika kuhakikisha mazingira bora kwa wawekezaji kwa kutatua changamoto zinazowakabili.
Katika mazungumzo hayo Leodegar Tenga amesema kuwa lengo la kukutana na Mhe. Waziri ni kueleza Majukumu ya Shirikisho ambayo ni kusukuma Maendeleo ya Viwanda nchini.
Leodegar Tenga ametoa ahadi kwa Serikali ya kuunga mkono mipango ya nchi kutumia Viwanda kama mhimili wa uchumi na kuhamasisha matumizi ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya Nchi. Ameeleza kuwa, CTI inaishukuru Serikali ya awamu ya tano ambayo imetilia mkazo Maendeleo ya Viwanda nchini.
“Nimefarijika Sana kwa mawazo kutoka kwa Mhe. Waziri na nna imani Mhe. Mwambe atatufikisha katika malengo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda kama ilivyo kauli mbiu ya Rais wetu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli” Leodegar Tenga.
Katika kikao hicho kilichofanyika ofisi za Wizara Mtumba, ndugu Leodegar Tenga amekabidhi kwa waziri wa Viwanda na Biashara, 1. Mpango mkakati wa kuendeleza Viwanda nchini, 2. Kanuni za maadili ya wanachama wa Shirikisho la wenye Viwanda nchini (CTI) na
3. Jarida ambalo linatangaza mafanikio ya serikali na azma ya kujenga Tanzania ya Viwanda, mchango wa Serikali kuendeleza Viwanda na kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini.