Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega akigawa zawadi ya mipira kwa uongozi wa Shule ya Sekondari Dodoma kwa ajili ya shughuli za michezo shuleni hapo, wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli za michezo shuleni hapo Januari 27, 2021 Jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Antony Mavunde, uongozi wa Jiji hilo pamoja na wanafunzi wa shule hiyo.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega akisalimiana na wanafunzi wa shule ya michezo ya Fountain Gate Academy ambao ni wanamichezo waliotwaa ubingwa wa mpira wa miguu wavulana na wasichana chini ya umri wa miaka 15 (U15) katika mashindano ya East Africa Chipukizi Cup 2020 ambayo yalifanyika Mkoani Arusha.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega akirusha mpira pamoja na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Antony Mavunde, kuashiria ufunguzi wa mechi ya mpira wa pete kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli za michezo shuleni hapo Januari 27, 2021 Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega akicheza kwaya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma waliotumbuiza wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli za michezo shuleni hapo Januari 27, 2021 Jijini Dodoma.
*************************************************
Na Shamimu Nyaki – WHUSM, Dodoma
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Ulega ameagiza viongozi na wasimamizi wa shule zote nchini kusimamia vyema vipindi vya michezo shuleni.
Mhe. Ulega ameyasema hayo leo Januari 27, 2021 katika ziara yake ya kukagua shughuli za michezo shuleni, ambapo alitembelea Shule ya Sekondari Dodoma pamoja na Shule ya ya Michezo ya Fountain Gate.
Akizungumza alipokua shule ya Sekondari Dodoma, Mhe. Naibu Waziri Ulega ameipongeza shule hiyo kwa kuwa na ratiba ya vipindi vya michezo ambayo inatekelezwa, ambapo amesisitiza ratiba hiyo iendelee kuzingatiwa.
“Vipindi vya michezo shuleni viheshimiwe, wanafunzi wapate nafasi ya kucheza ili waimarishe afya zao, pia wakuze na kuendeleza vipaji vya michezo mbalimbali ambavyo vitawasaidia katika maisha yao baada ya shule pamoja na kulitumikia Taifa katika Sekta ya michezo”, alisema Mhe.Ulega.
Aidha, Mhe. Ulega amewataka watanzania kuendelea kuiunga mkono timu ya Taifa inayoshiriki mashindano ya CHAN huko nchini Cameroon, ambapo amewasihi watanzania kuacha kuishambulia timu hiyo bali waiunge mkono kwa kuwa ndio iliyoaminiwa kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo.
Mhe. Ulega ameongeza kuwa Mikoa na Halmashauri zote lazima zitenge fedha kidogo katika bajeti zao kwa ajili ya kuwezesha majukumu ya Maafisa Michezo na Utamaduni katika maeneo yao.
Awali Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Maduka Kessy ameeleza kuwa michezo katika mkoa huo inaenda vizuri, huku akitolea mfano timu ya Dodoma Jiji inayoshiriki ligi kuu pamoja na Dodoma Queens inayoshiriki ligi ya wanawake.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuahidi kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya michezo, tunaahidi tutaitumia vizuri katika kuendeleza michezo hapa mkoani na nchi kwa ujumla” alisema Dkt. Kessy.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari Dodoma, Bw. Amani Mfaume amesema shule hiyo ni kituo cha michezo kwa mkoa wa Dodoma na imekuwa ikifanya vizuri katika michezo mbalimbali inayofanyika kila mwaka.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alitembelea Shule ya Fountain Gate Academy ambapo pamoja na kujionea shughuli za michezo zinazofanyika shuleni hapo aliagiza shule hiyo kuwa Mawakala wa wachezaji lengo ni kuwa kituo bora cha kusajili wachezaji kwenye vilabu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Tunataka shughuli za uwakala wa wachezaji zitambulike rasmi ili zichangie katika kukuza michezo pamoja na kuchangia katika pato la taifa, pia tuweze kuzalisha ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi”, alisisitiza Mhe. Ulega.
Ziara ya Mhe. Ulega itaendela katika Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.