Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi Prof. Evaristo Liwa (wa tatu kutoka kulia) akisisitiza jambo kwa Menejimenti ya Wizara ya Ardhi wakati wa kikao cha pamoja cha kujadili kuhusu utekelezaji wa majukumu ya iliyokuwa Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Bi. Mary Makondo na Naibu wake Bw. Nicholas Mkapa
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Mary Makondo akiteta jambo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Ardhi, Prof. Evaristo Liwa katika kikao cha pamoja kilichofanyika jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Bw. Hamdouny Mansour (aliyeshika karatasi) akimuonesha Prof. Evaristo Liwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi ramani ya eneo zilipo ofisi zilizokuwa zikitumiwa na iliyokuwa Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA).
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Bi. Mary Makondo akimkabidhi Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Prof. Evaristo Liwa Hatimilki ya kiwanja kilichokuwa kinamilikiwa na iliyokuwa Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA)Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Bi. Mary Makondo akimkabidhi funguo za majengo na ofisi zilizokuwa zinatumiwa na iliyokuwa Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi, Prof. Evaristo Liwa.
**************************************************
Na Eliafile Solla
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Mary Makondo amekerwa na baadhi ya watendaji wa umma kutokuwa na uchungu na uharibifu wa mali za Serikali katika maeneo wanayosimamia.
Hali hiyo ilijitokeza mwanzoni mwa wiki wakati Bi. Mary alipofanya ziara katika ofisi zilizokuwa zikitumiwa na Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA – National Housing and Building Research Agency) zilizopo maeneo ya Mwenge Jijini Dar es Salaam na kukuta baadhi ya mali zimeharibiwa na sehemu ya ukuta wa uzio ukiwa umevunjwa huku kukiwa na walinzi.
Bibi Mary alisema, kusimamia mali za Serikali zikiharibiwa ni kosa kama yalivyo makosa mengine ya jinai na hivyo ni lazima kila aliyehusika na uzembe huo awajibike. Alimuagiza kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa haraka kwa wote waliohusika na uharibifu huo katika eneo la Serikali.
Katika ziara hiyo, Bi. Mary alikuwa na timu ya Menejimenti ya Wizara na viongozi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) wakiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Evaristo Liwa ambapo walipata wasaa wa kujadili mambo kadha wa kadha kuhusu iliyokuwa Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi na baadae kwenda kukagua ofisi na mali zilizokuwa zinamilikiwa na wakala huo.
Lengo la ziara hiyo ilikuwa kukabidhiana ofisi baada ya Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi ambayo ilikuwa chini ya Wizara ya Ardhi kuvunjwa rasmi na majukumu yake ya kufanya tafiti kuelekezwa katika Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) tangu mwezi Aprili 2020.
Mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, zilifanyika juhudi za kupunguza ukubwa wa Serikali kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza tija na ufanisi wa Serikali. Katika mchakato huo uliosimamiwa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, ilibainika kuwa majukumu mengi ya Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) yangeweza kutekeleza kwa ufanisi na umakini zaidi endapo yangetwaliwa na Vyuo vikuu ambavyo kimsingi kazi za kitafiti ndilo jukumu lake kuu.
Hivyo Serikali kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi ilifanya uchambuzi wa kina uliohusisha vyuo vikuu na baadhi ya mashirika ya Serikali kama vile; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), DIT, SIDO, VETA na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) na hatimae ikaonekana kuwa ARU ndiyo Taasisi sahihi ya kurithi majukumu na kazi zilizokuwa zikitekelezwa na Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA).