Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Hole Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati
………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu,
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini TAKUKURU Mkoani Manyara imetoa onyo kwa wafanyabiashara wa madini ya tanzanite wa Mji mdog wa Mirerani Wilayani Simanjiro wanaoendelea kutorosha madini hayo bila kulipa tozo za Serikali.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara Holle Joseph Makungu, ametoa onyo hilo alipokuwa akitoa taarifa ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita kwa waandishi wa habari Mjini Babati.
Makungu amesema kuwa kuna baadhi ya wafanyabishara wanaendelea kutorosha madini hayo kwa kukwepa kulipa tozo za serikali, kitendo ambacho ni kinyume cha kanuni za madini za mwaka 2019.
Hata hivyo, amesema Mkuu wa TAKUKURU wa kituo maalumu cha Mirerani Sultan Ngaladzi na Ofisa madini mkazi wa Mkoa wa kimadini wa Mirerani, Fabian Mshai wamekuwa wakitoa elimu kwa wadau wa madini ya hayo Tanzanite.
Amesema katika semina hizo wamewatahadharisha juu ya ukiukwaji wa usafirishaji wa madini ambapo taarifa za kiintelejensia zinaonyesha kuwa walijitokeza wafanyabiashara wa nje wasio waaminifu ambao wamekuwa wakichepusha madini ya Tanzanite na kuyapeleka masoko ya nje ya nchi badala ya kuyapeleka kwenye masoko ya ndani yaliyofunguliwa na Serikali kwa shughuli hiyo.
“Kwa mujibu wa kanuni ya 12 ya usafirishaji wa madini ya mwaka 2019 wafanyabiashara wanapaswa kufanyiwa tathimini ya madini yao na kulipia mrahaba, tozo ya ukaguzi na tozo ya huduma katika kituo maalumu cha ukaguzi kikichopo jengo la one stop centre Mirerani, ” amesema Makungu.
Aidha mkuu huyo wa TAKUKURU Manyara amezitaka tasisi zinazodaiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme TAMESA mkoani Manyara kulipa madeni yao haraka kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita TAKUKURU Manyara imefanikiwa kuwarejeshea fedha na mali mbalimbali baadhi ya watu waliokuwa wamekopeshwa mikopo isiyo na lesenimikopo umiza, imetoa elimu ya rushwa mashule na imedhibiti miradi 11 ya zaidi ya shilingi bilioni 1 iliyokuwa kwenye mazingira ya kuhujumiwa.
Pia Taasisi hiyo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Manyara, imeanzisha ofisi inayotembea maarufu PCCB mobile ambayo inawafuata wananachi maeneo yao na kusikiliza kero zao.