*****************************************************
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Kampuni ya Jackson Group Sport kwa kushirikiana na Shirikisho la Ngumi la Dunia (WBF) limeandaa semina ya siku moja kwa waamuzi na majaji wa Tanzania ili kuwawezesha kujua sheria mbalimbali.
Semina hiyo itafanyika Jumanne (Januari 26) kwenye hotel ya Onomo ya Dar es Salaam na kushirikisha mashiriki 20 kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa.
Twissa alisema kuwa rais wa WBF, Howard Goldberg ataendesha semina hiyo ambayo ni moja ya mikakati ya kampuni yao kuinua mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.
Alisema kuwa semina hii ni jambo lao la pili tokea kuanza kuandaa ngumi za kulipwa nchini na moja ya kuhamasisha maendeleo ya mchezo huo kulekea pambano lao la Ijumaa kwenye ukumbi wa Next Door Arena ambapo bondia Ibrahim Class atapambana na Dennis Mwale wa Malawi kuwania mkanda wa mabara wa uzito wa super feather wa WBF.
Twissa alisema kuwa Goldberg ana uzoefu wa miaka zaii ya 40 kwenye masuala ya ngumi za kulipwa duniani na ameweza kuendesha semina kama hizo kwa nchi zaidi ya 15 pamoja na Ghana, Afrika Kusini, Misri, Gabon na Zimbabwe kwa upande wa Afrika.
“Wakati tunaendelea kuinua viwango vya mabondia nchini, tumeaona pia kuongezea uwezo waamuzi na majaji ili kuweka kufanya kazi yao vizuri. Mara kadhaa nimesema kuwa tunachokisema ndicho tunakifanya nah ii ni moja ya majukumu yetu,” alisema Twissa.