Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Agostino Maneno wa sita kutoka kushoto aliyevaa shati la mikono,Mganga Mkuu wa wilaya ya Tunduru Dkt Wendy Robert wa tano na Mratibu wa tano kutoka kulia wakiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu(Res Cross) baada ya mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo wanachama hao ya kuibua na kutokomeza Ugonjwa wa kifua Kikuu katika wilaya hiyo inayotajwa kuongoza kuwa na wagonjwa wengi ikilinganisha na wilaya nyingine katika mkoa wa Ruvuma.
Picha na Muhidin Amri
……………………………………………………………………….
Na Muhidin Amri,Tunduru
HOSPITALI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imezindua rasmi kampeni ya kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu mwaka 2021 kwa kuanza kuwatumia wanachama wa chama cha Msalaba mwekundu(Red Cross) kama mkakati wake utakaowezesha kupunguza maambukizi na kuwaibua watu wengi wanaougua ugonjwa huo.
Wanachama hao,wataungana na wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma wa Hospitali ya wilaya katika kutokomeza ugonjwa huo ambapo kwa mkoa wa Ruvuma wilaya hiyo inaongoza kwa maambukizi makubwa ya kifua kikuu.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole amesema, wameamua kuwatumia na kuwashirikisha wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu kutokana na umuhimu wao katika jamii kwa kuwapa mafunzo ambayo yatawasaidia kushiriki vyema katika mapambano ya ugonjwa huo.
“uzinduzi wa mapambano ya kifua kikuu katika wilaya yetu kwa mwaka 2021 tumeanza na wanachama wa chama cha Msalaba Mwekundu kutokana na ukaribu wao na jamii, kwa hiyo tumelazimika kuwapa elimu kwa kuamini kuwa tutaongeza kasi ya kuwaibua wagonjwa wengi zaidi wa kifua kikuu katika wilaya yetu kama ilivyokuwa mwaka2020”alisema.
Alisema, uzinduzi huo utakwenda sambamba na kufanya kampeni ya kuelimisha na kuchunguza vimelea vya ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali ikiwemo taasisi za serikali,shule kwa shule, nyumba kwa nyumba na kwenye vilinge vya waganga wa Tiba asili na tiba mbadala.
Dkt Mkasange alisema, wale watakaobainika kuwa na ugonjwa huo wataanzishiwa dawa zinazotolewa bure katika zahanati,vituo vya Afya na Hospitali zote na kuiomba jamii kushirikiana katika kampeni ya mwaka huu.
Kwa mujibu wa Dkt Mkasange, kauli mbiu ya kampeni ya kifua kikuu mwaka 2021 ni Tb katika wilaya ya Tunduru ni ya watu wote kwa kila mmoja ana wajibu kutokomeza ugonjwa huo.
Akizindua kampeni hiyo mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Tunduru Agostino Maneno, amewapongeza wanachama wa chama cha Msalaba Mwekundu kwa kukubali kuwa sehemu ya timu ya kampeni ya kutokomeza ugonjwa huo na kuwataka kwenda kushiriki kikamilifu katika kuwaibua wagonjwa wengi wa kifua kikuu.
Alisema, lengo la serikali siku zote ni kuboresha afya za wananchi wake na kuwataka watendaji wa vijiji,mitaa na kata kuwapa ushirikiano wanachama hao pale wanapofika katika maeneo yao kwa ajili ya kutekeleza kazi hiyo kwani wanakwenda kuongeza nguvu ya kuibua watu wengi na kuzuia kuongezeka kwa maambukizi ya kifua kikuu.
Maneno alisema, kimsingi kampeni yay a kutokomeza kifua kikuu sio ya mtu mmoja au kikundi fulani cha watu, bali kila mtu anawajibu wa kushiriki kwa kuibua,kutokomeza na kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo unaotajwa kati ya magonjwa 10 Duniani yanayoongoza kuuwa watu wengi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Tunduru Dkt Wendy Robert alisema, kuna mikakati mbalimbali ya kuibua wagonjwa wengi zaidi wa kifua kikuu na mwaka huu wameanza kutoa elimu kwa wanachama wa Red Cross na kuendelea kuwajengea uwezo makundi mbalimbali yakiwemo Waganga wa tiba asili,watoa huduma ngazi ya jamii.
Alisema, mwaka huu nguvu kubwa itatumika katika kuibua wagonjwa wa kifua kikuu hasa baada ya kuona katika wilaya hiyo kuna wagonjwa wengi wa kifua kikuu.
Dkt Wendy alisema, mwaka jana mkakati ni kuwaibua wagonjwa 647,hata hivyo kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na wataalam wa kitengo cha kifua kikuu Hospitali ya wilaya na wadau wengine kupitia kampeni mbalimbali walifanikiwa kuibua watu 704.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Salome Golihama alisema, kupitia mafunzo hayo jamii itarajie kupata elimu kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu na watahakikisha wanashiriki vyema katika mapambano ya kutokomeza ugonjwa huo.