Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita wa shule ya Sekondari ya Wavulana Songea(Songea Boys) wakimsikiliza Afisa Huduma na Elimu kwa walipa kodi wa Mamlaka ya Mapato(TRA)Mkoa wa Ruvuma Justine Katiti(hayupo pichani) wakati wa Utoaji wa Elimu ya kodi kwa wanafunzi hao iliyofanyika katika ofisi za Mamlaka hiyo ambapo Tra inatoa Elimu ya kodi katika shule mbalimbali za msingi na Sekondari mkoani humo.
Picha na Muhidin Amri
…………………………………………………………………………………….
Na Muhidin Amri,Songea
MAMLAKA ya mapato(TRA)mkoani Ruvuma,imeanza kutoa elimu ya walipa kodi kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za Sekondari katika mkoa huo yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya kodi ili wanapomaliza masomo yao wawe walipa kodi na kuwa wawakilishi wazuri katika masuala ya kodi.
Afisa huduma na elimu kwa walipa kodi mkoa wa Ruvuma Jastine Katiti alisema,wako katika utaratibu wa kutoa elimu kwa walipa kodi hususani katika makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo kuanzisha klabu za walipa kodi(Tax club) kwa shule zote za sekondari.
Alisema, lengo ni kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na uelewa mkubwa katika masuala mbalimbali ya kodi ili baada ya kumalia masomo yao wawe walipa kodi ,wakusanya kodi na walimu wazuri katika masuala mbalimbali yanahusu kodi za serikali.
Alisema,kila mwaka wanatoa elimu ya kodi kwa wanafunzi wa shule sita katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma, na utaratibu uliopo katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza wanatembelea shule tatu na wakati mwingine wanafunzi wanafika kwenye ofisi za Tra ili kupata elimu ya kodi kama sehemu ya masomo yao.
Alisema ni mategemeo ya Tra kuwa,wanafunzi hao pindi watapomaliza masomo yao watakuwa wawakilishi wazuri na walipa kodi ambao watafanya shughuli zao bila kificho au kukimbia wanapowaona maafisa wa Tra.
Baadhi ya wanafunzi waliopata elimu ya kodi kutoka shule ya Wavulana Songea wameipongea Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato nchini kwa kazi nzuri inayofanya ya kukusanya mapato ya Serikali ambayo yamesaidia sana nchi kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
Emmanuel Malagwa mwanafunzi wa kidato cha sita alisema, sasa watanzania wanatembea kifua mbele kutokana na maendeleo makubwa, kukua kwa uchumi,kupungua kwa umaskini na kuimarika kwa huduma mbalimbali za kijamii.
Alisema, mafanikio hayo yamepatikana kutokana na mchango mkubwa unaofanywa na watumishi wa mamlaka ya mapato kukusanya kodi na maduhuli mengine ya serikali.
Aidha, amewataka watanzania kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tra katika suala zima la kulipa kodi na ukusanyaji mapato ya Serikali kwani matunda yake yameanza kuonekana katika maeneo mbalimbali ya nchini na kuhaidi kuanzia sasa na hata watakapomaliza masomo yao watakuwa mabalozi wa kuitangaza vyema serikali na kuwa walipa kodi wazuri.
Ronaldo Adam,amempongeza Rais Dkt John Magufuli kwa kazi nzuri ya kusimamia suala ulipaji wa kodi ambazo kwa kweli mchango wake ni mkubwa ambapo kati ya kazi nzuri ya kukusanya kodi ni ukarabati mkubwa wa majengo katika shule ya Sekondari ya Wavulana Songea.
Alisema, suala la ulipaji kodi sio jambo la mtu au idara moja ya Serikali, bali kila mtu ana wajibu na kuhakikisha analipa kodi za Serikali na kuwataka wazazi na jamii kulipa kodi kwa wakati tena bila shuruti.
Ameiomba serikali kupitia Tra kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa jamii juu na kutumia vyombo vya habari ili elimu ya ulipaji kodi iwafikie watu wengi,badala ya kujikita zaidi katika maeneo ya mjini ambako watu wengi wameshaelewa maana ya kulipa kodi.
Amemuomba Rais Dkt John Magufuli na wasaidizi wake wa nafasi mbalimbali katika utumishi wa umma,kufanya kazi usiku na mchana na kutovunjika moyo kutokana na maneno ya baadhi ya watu wakiwemo wana Siasa uchwara wasioitakia mema nchi yetu.